WATUMISHI WA WIZARA WAHIMIZWA USHIRIKIANO

Imewekwa: Wednesday 16, December 2020

Waziri Mteule wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha sekta hizo mbili zinachangia kwa sehemu kubwa katika maendeleo ya nchi na watu wake.

Ndaki ameyasema hayo alipokuwa akiongea na Viongozi pamoja na Watumishi wa wizara hiyo muda mfupi baada ya kuwasili kuanza kazi katika ofizi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Disemba 10, 2020.

Akiongea na Watumishi hao, Ndaki alisema anaamini kuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana baina ya viongozi na watumishi wataweza kufikia malengo ya Wizara ya kuhakikisha inatoa mchango mkubwa katika pato la taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Mhe. Rais ametupa maelekezo mengi kuanzia katika hotuba yake ya kufungua bunge na hata alipokuwa anatuapisha jana Disemba 9, 2020 alirudia maelekezo yake kwetu ya kwamba tukahakikishe sekta hizi mbili zinatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Ndaki

Aliongeza kuwa watanzania wana matarajio makubwa kwao na ushirikiano pekee ndio utakaowawezesha kufanya kazi zao vizuri na kufikia matarajio ya wananchi ya kuwaletea maendeleo.

Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema kuwa wao wamekwenda Wizarani hapo kuongeza nguvu ili kutimiza matarajio ya Watanzania huku akiwataka watumishi kushikamana kuhakikisha wanafikia adhma hiyo.

“Naomba tushikamane, tushirikiane tutimize ndoto ya Rais, hatuna budi kukimbia sana huko katika maeneo ya kazi ili watanzania waone wanahudumiwa vizuri,” alisema Gekul

Awali, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alimpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kuteuliwa kuwa viongozi katika wizara hiyo kwani wanaamini ujio wao utasaidia kurahisisha utendaji wa kazi katika kuwahudumia wananchi katika kipindi cha miaka mitano (5) ijayo.

.