Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
Idara ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo
IDARA YA UENDELEZAJI WA ARDHI YA MALISHO NA RASILIMALI ZA VYAKULA VYA MIFUGO
MAJUKUMU YA IDARA
- Kusimamia uzalishaji wa mbegu za malisho na malisho katika mashamba ya Vikuge na Langwira;
- Kushrikiana na wadau wengine kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na uainishaji wa maeneo ya malisho;
- Kutoa ushauri wa kitaalam kwenye maandalizi ya mipango ya matumizi ya ardhi pamoja na usajili wa maeneo ya malisho;
- Kusimamia uanzishwaji na uboreshwaji wa maeneo ya malisho kwa uzalishaji endelevu;
- Kuratibu na kusimamia kazi za wakaguzi wa maeneo ya malisho na vyakula vya mifugo;
- Kusimamia na kutoa Kanuni na Miongozo ya uzalishaji, uhifadhi, uingizaji na utoaji wa malisho, mimea malisho na mbegu za malisho ndani na nje ya nchi;
- Kuhamasisha na kuwezesha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji kwa ajili ya mifugo;
- Kuhamasisha na kusimamia Sera na Mifumo ya uzalishaji wa mifugo kwa jamii za wafugaji wa asili;
- Kuhamasisha na kuimarisha ustawi wa jamii za wafugaji wa asili ili kuzuia migogoro na watumiaji wengine wa ardhi;
- Kuhamasisha na kusimamia uzalishaji na biashara ya raslimali za vyakula vya mifugo; na
- Kuratibu na kusimamia utoaji wa vibali vya kusafirisha vyakula vya mifugo kwa mfumo wa kieletroniki wa MIMIS.
MALISHO
UTANGULIZI
Malisho ni lishe ya msingi kwa mifugo kinachojumuisha aina mbalimbali za nyasi na mikunde. Utunzaji wa malisho ni muhimu ili kuhakikisha kwamba mifugo inapata virutubisho vinavyohitajika. Ukuaji na ustawi wa aina za malisho hutofautiana kutegemea hali ya hewa na mazingira mbalimbali.
UZALISHAJI WA MALISHO
- Andaa shamba
- Chagua aina ya malisho unayokusudia kupanda kufuatana na aina ya udongo na hali ya hewa
- Panda mbegu bora kufuatana na aina ya malisho (mbegu, vipingili, vishina au chipukizi). Mbegu bora zipandwe kwa ekari kilo 5-10 kwa nyasi na kilo 2-6 kwa mikunde kutegemea aina ya mbegu
- Ondoa magugu kupunguza ushindani wa maji, hewa na mwanga kati ya malisho na magugu
- Weka mbolea ya samadi, mboji au ya viwanda kama NPK, CAN, TSP kwa kufuata ushauri wa mtalaamu wa mifugo
- Hakikisha malisho yanapata maji ya kutosha
AINA ZA MALISHO
Malisho yamegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni nyasi na mikunde.
Baadhi ya aina ya nyasi ni:
a)Buffel grass/African foxtail (Cenchrus ciliaris)
Sifa;
•Huvumilia ukame na zinahimili kuchungwa.
•Mahitaji ya mvua kuanzia milimita 300 hadi 750
•Huwa na protini kiasi cha asilimia 6-7 mara baada ya kuchanua maua.
•Hustawishwa kwa mbegu au vichipukizi.
•Yanaweza kutumika kuchingia mifugo au kutengeneza hei
•Mavuno ni kuanzia tani 6 hadi 10 za majani makavu (DM) kwa ekari kwa mwaka
b)Rhodes grass
- Hustawi katika maeneo yanapopata mvua za wastani hadi nyingi (mm 600-1200),
- Hupandwa kwa kutumia mbegu,
- Mbegu zake ni ndogo hivyo huchanganywa na mchanga wakati wa kupanda,
- Huweza kuchanganywa kwa kupandwa na majani jamii ya mikunde kama Desmodium au Siratro,
- Kiasi cha protini ni wastani wa 10% kutegemeana na aina ya udongo, matumizi ya mbolea na kipindi cha kuvuna.
c)Guatemala (Tripscum Laxum)
- Hustawishwa kwa chipukizi kwa nafasi kati ya mashina
- Hustawisha vizuri kwenye eneo lenye mvua za wastani
- Huvunwa yakiwa na urefu wa mita moja na robo na hukatwa sentimeta 15 kutoka usawa wa ardhi
- Kiasi cha protini ni wastani wa 7% kutegemea aina ya udongo na matumizi ya mbolea.
d)Napier grass (Juncao)
- Hustahimili ukame
- Huhutaji mvua za wastani kuanzia milimita 600 hadi 1,500 kwa mwaka
- Upandaji wake ni mita 1 moja kati ya mstari na mita 1 kati ya mashina
- Kiasi cha protini ni wastani wa asilimia 10 hadi 12 kutegemea na aina ya udongo, matumizi ya mbolea na kipindi cha kuvuna
- Mavuno huweza kufikia tani 150 hadi 200 za majani mabichi kwa ekari kwa mwaka
JAMII YA MIKUNDE
a)Alfaalfa (Medicago sativa)
- Hustahimili ukame
- Huhutaji mvua za wastani kuanzia milimita 400 hadi 1,500 kwa mwaka
- Yanaweza kutumika kuchingia mifugo au kutengeneza hei au Saileji
- Mavuno ni tani 8 hadi 15 za majani makavu kwa ekari kwa mwaka
UHIFADHI WA MALISHO
UTANGULIZI
Malisho ndio chakula kikuu cha mifugo inayocheua (ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda na ngamia. Malisho hupatikana kwa wingi wakati wa masika ambapo wakati huo huwa na ubora wa kutosha na hivyo kukidhi mahitaji ya maifugo. Aidha wakati wa kiangazi malisho huwa kidogo na viini lishe hupungua. Ili kuhakikisah upatikanaji wa malisho wakati wote wa mwaka na yenye ubora, ni muhimu kuhifadhi malisho ya ziada wakati wa masika. Njia mojawapo ya kuhifadhi malisho haya ni pamoja na kuyakausha yaani Hei au kuhifadhi kama Saileji.
Hatua za kuandaa Hei
Vuna majani mara tu yanapoanza kutoa maua kwani wakati huu viinilishe vinakuwa katika kiwango cha juu
Yakaushe kwa kuyageuza geuza mara moja hadi mbili kwa siku. Ukaushaji huchukua siku tatu hadi sita kutegemeana na aina ya majani au hali ya hewa.
Yakikauka yafunge kwenye marobota
Hifadhi marobota sehemu isiyoingiza mvua au unyevu
Marobota yanaweza kutengenezwamashine au kwa kasha la mbao
Mfugaji mwenye uwezo mdogo anashauriwa kutumia kasha la mbao
Makasha ya mbao yanaweza kutengenezwa kwa kutumia vipimo vifuatavyo:
Kasha linaweza kuwa na urefu wa sentimita 75, upana sentimita 45 na kina sentimita 35. Majani yaliyofungwa Kwenye marobota hutumia sehemu ndogo ya kuhifadhi na pia hupunguza upotevu
JINSI YA KUFUNGA MAROBOTA
a) Tengeneza kasha | b) Weka kamba nne kwenye kasha | c) Weka hei kwenye kasha halafu Shindilia | d) Funga majani/ robota | e) Ondoa robota kwenye kasha |
f) Hifadhi marobota katika banda
Hei pia inaweza kuhifadhiwa shambani (ngitiri, olalii). Malisho huachwa shambani bila kuchunga mifugo ili yaweze kuwa akiba wakati wa kiangazi. Ng’ombe wanaweza kuruhusiwa kuchunga shambani moja kwa moja au kukata na kulishia nyumbani. Hata hivyo hei iliyohifadhiwa shambani huwa na viinilishe kidogo kwa sababu majani yanakuwa yamekomaa sana.
Kumbuka:
Kwa wale ambao hawana uwezo wa kutengeneza kasha wanaweza kuvuna na kukausha kisha kuhifadhi ndani ya ghala/chumba cha kuhifadhia malisho.
UHIFADHI WA MALISHO KWA TEKNOLOJIA YA SAILEJI
Saileji ni majani yaliyokatwakatwa na kuhifadhiwa kwa kutumia mchakato wa uchachuaji (fermentation) ili yaweze kutumika kwa muda mrefu bila kuharibika. Hutengenezwa kwa kuhifadhi nyasi, matama, mahindi, au mimea mingine ya malisho katika hali ya unyevunyevu ndani ya mazingira yasiyo na hewa (anaerobic), kama vile kwenye mashimo (silo pits), mifuko maalum, au matanki ya kuhifadhia. Saileji ni muhimu kwa ufugaji kwani ina virutubisho vya kutosha kwa mifugo hasa wakati wa ukame,husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama na pia ni njia bora ya kuhifadhi malisho kwa muda mrefu.
NJIA YA UTENGENEZA WA SAILEJI
Mchakato wa kutengeneza sailage umegawanyika katika hatua kadhaa. Unapaswa kufanya mpango sahihi na kutengeneza kulingana na mahitaji yako.
a) Kata malisho kwa kutumia mashine | b) Kata malisho kwa kutumia panga | c) Malisho yaliyokatwa vipande vidogo vidogo | d) Changanya maji na molasesi | e) Gandamizakuondoa hewa kwa kutumia pipa lililojaa maji |
Gandamiza kuondoa hewa kwa kutumia trekta | Funika kwa kutumia nailoni maalumu | Utengenezaji wa Saileji kwa kutumia nailoni maalumu | Saileji iliyokamilika kutengenezwa |
Hatua kwa hatua juu ya utengenezaji wa silage
- Chagua sehemu salama na kavu ya kuchimba shimo. Chagua mahali kwenye ardhi yenye mteremko kidogo na kina cha shimo kipungue kutoka upande wa juu wenye mteremko hadi upande wa chini kwa kutoa umbo kama pembe tatu.
- Baada ya kutengeneza shimo, vuna malisho na ukate vipande vidogo vidogo kwa kutumia mashine au panga. Kata malisho katika vipande vyenye urefu wa inchi moja;
- Funika sehemu ya chini ya shimo kwa karatasi ya nailoni ili kuzuia saileji kugusana na udongo. Pia funika pande zote za shimo, kisha weka malisho yaliyokatwa ndani ya shimo
- Changanya lita moja ya molasesi kwa lita tatu za maji. Na kuinyunyiza sawasawa kwenye malisho. Tumia bomba kunyunyuzia mchanganyo uliotengeneza hapo juu.
- Kisha kandamiza malisho kwa miguu au kwa kutumia kitu kizito (dram au trekta) kwa ajili ya kutoa hewa nje na kulinda malisho kutokana na mashambulizi ya ukungu.
- Funika sehemu ya juu ya shimo kwa karatasi ya nailoni baada ya kukandamiza mara ya mwisho. Funika juu ni muhimu ili kuzuia saileji kulowana na maji, ikiwezekana chimba mfereji mdogo pande zote za shimo ili kuondoa maji kwenye malisho.
- Subiri angalau siku 21 kabla ya kutumia saileji, saileji iliyotengenezwa kwa mchakato kama huo inaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu, kwa ujumla hadi miaka miwili.
- Fungua shimo kutoka upande wa chini wenye mteremko kama unahitaji kutumia saileji; na kisha chukua saileji ya kutosha kwa siku moja na ufunge shimo tena. Rudia utaratibu huo kila unapohitaji saileji kwa ajili ya kulisha mifugo yako.
MIUNDOMBINU YA MAJI YA MIFUGO
UTANGULIZI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina jukumu kubwa la kuhakikisha inasimamia ustawi wa Sekta ya Mifugo kwa kuboresha mazingira wezeshi ya Wafugaji na Mifugo yao kwa kuweka miundombinu ya Maji ya kutosha na ya uhakika.
HALI HALISI YA MAJI KWA SASA
Upatikanaji wa maji kwa sasa hautoshelezi idadi ya mifugo iliyopo kwa sasa hali inayosababisha kuwepo kwa changamoto ya mifugo kuhamahama ili kutafuta maji na malisho.
Changamoto ya maji na malisho husababisha migongano ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
WITO WA WADAU WA MAENDELEO
Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye maeneo ya wafugaji kwa lengo la kupunguza changamoto ya uhaba wa maji kwa mifugo. Hata hivyo, uhitaji wa maji kwa mifugo ni mkubwa ukilinganisha na miundombinu ya maji iliyopo. Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana katika kuboresha mazingira ya ufugaji kwa kuhakikisha upatikanaji wa malisho na maji. Ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na jamii za wafugaji ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya kuimarisha Sekta ya mifugo.
HATUA ZA UJENZI WA BWAWA LA MAJI
Kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji hasa mabwawa, zipo hatua mbalimbali za uandaaji wa michoro ya bwawa.
a)Anza kwa kuanda mchoro wa bwawa
Wasiliana na mhandisi kuandaa mchoro wa bwawa la maji kwa ajili ya mifugo
b)Kubaini eneo la kuchimba bwawa
Eneo la kuchimba bwawa linatakiwa liwe katika eneo lenye maji yanayotiririka kipindi cha mvua na likubalike kwa jamii inayolizunguka
c)Uchimbaji wa bwawa
Safisha mahali pakujenga bwawa. Kupima ukubwa wa bwawa Kuondoa udongo wa juu (mbolea, mchanga, mizizi n.k.) na kuweka pembeni. Kuchimba msingi wa kuta; upana futi 1 na kina futi 1½. Kujaza huo msingi kwa udongo wa mfinyanzi na kuushindilia
UZALISHAJI WA MBEGU ZA MALISHO NA MALISHO
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inasimamia mashamba maalum ya uzalishaji wa mbegu bora za malisho na malisho kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu za malisho hapa nchini. Mamshamba hayo ni:-
- Shamba la Vikuge – Lipo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
- Shamba la Langwira – Lipo Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.
Mbegu za malisho zinazozalishwa katika mashamba hayo ni pamoja na mbegu aina ya nyasi kama kama Cenchrus ciliaris, Chloris gayana, Panicum spp (Super Napier, Juncao) na mikunde kama Tropical kudzu na Centrocema pubescens.
Wizara inaendelea na jitihada za kuboresha mashamba haya kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za malisho bora kwa wafugaji nchini.