Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MEENA ATAKA USHIRIKIANO, TAASISI SITA ZA MIFUGO KUWA JENGO MOJA

Imewekwa: 22 October, 2025
MEENA ATAKA USHIRIKIANO, TAASISI SITA ZA MIFUGO KUWA JENGO MOJA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amezitaka taasisi sita kutoka sekta ya mifugo zinazojenga ofisi zake katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, kusimamia ujenzi huo kwa ushirikiano ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyotarajiwa.

Bi. Meena amebainisha hayo Oktoba 21, 2025 kwenye tukio la utiaji sahihi wa mkataba wa ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya taasisi hizo, zilizo chini ya wizara na kukabidhi eneo kwa mkandarasi wa ujenzi wa jengo hilo, ambapo amesema kukamilika kwa ujenzi kutasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa ofisi bora kwa watumishi.

Akizungumzia juu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambazo zitakuwa kwenye jengo moja, amesema anatambua TALIRI ndiyo imeingia makubaliano ya kimkataba lakini taasisi zingine tano zisijiweke kando bali zishiriki katika kusimamia ujenzi huo.

Aidha, amemtaka mkandarasi wa ujenzi Kampuni ya CJIETC kutoka China na mkandarasi mshauri wa ujenzi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kwa bidii na umahiri mkubwa ili ujenzi ukamilike kwa wakati na viwango vya juu kama ilivyoonyeshwa kwenye mkataba wa ujenzi wa miezi 24 pamoja na mwaka mmoja wa uangalizi.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wengine wa taasisi zitakazotumia jengo hilo baada ya kukamilika kwake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba, amesema wametumia mfumo ambao ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaratibu ujenzi wa majengo ya serikali jijini Dodoma, imeufurahia kwa taasisi hizo sita kutumia jengo moja katika eneo la ekari 10.

Pia, amesema ofisi ya Waziri Mkuu imesema itashawishi taasisi zingine zilizopo kwenye wizara mbalimbali kutumia mfumo huo wa kuwa na jengo moja, hivyo kurahisisha huduma kwa wananchi.

Naye Mkadiriaji Majenzi kutoka Kampuni ya CJIETC kutoka China Mhandisi Wencleaus Kiziba amesema watahakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa wakati na kulingana na bajeti ya fedha iliyotengwa pamoja na kuzingatia ubora.

Ujenzi wa jengo la ofisi za makao makuu ya TALIRI, TDB, LITA, TVLA, TMB na NARCO unatarajia kutumia takriban shilingi bilioni 54 zote kwa pamoja, ambapo mkandarasi atatekeleza kwa shilingi bilioni 49, TBA ambaye ni mshauri elekezi shilingi bilioni 4.5.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo