Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI ZIMEENDELEA KUBORESHA LISHE NCHINI-MAJALIWA

Imewekwa: 16 October, 2025
SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI ZIMEENDELEA KUBORESHA LISHE NCHINI-MAJALIWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa sekta za Mifugo na Uvuvi zimekuwa vinara kwenye mchango wa protini inayotokana na wanyama na samaki hapa nchini.

Mhe. Majaliwa amesema hayo Oktoba 16,2025 wakati akifunga Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani kwenye Viwanja vya  Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo imetokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali kwenye sekta hizo.

“kwa sasa uzalishaji wa nyama umefikia taribani tani laki 6 na mayai takribani milioni 7 huku upande wa Uvuvi uzalishaji wa samaki umefikia hadi zaidi ya tani laki 5 hivyo nitoe rai kwa wananchi kuhakikisha tunaendelea kuhakikisha tunazalisha, tunahifadhi na kutumia vyakula vyenye virutubisho vingi na vyenye ubora wakati wote” Ameongeza Mhe. Majaliwa.

Aidha Mhe. Majaliwa amewataka wananchi hususani wale wanaoishi vijijini kutumia Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kufanya maamuzi sahihi kuhusu lishe bora inayohitajika kutoka kwenye mazao yatokanayo sekta za na Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

“Hivi sasa kumekuwa na kasumba ya watu wengi kuwa na unene uliopitiliza hivyo ni lazima tuachane na mtindo wa kula kila kitu na badala yake tujielekeze kula chakula bora kama inavyoshauriwa na wataalam wa lishe”Amesema Mhe. Majaliwa.

Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amewaelekeza wataalam wa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuendelea kutumia mbinu bora za uzalishaji, uhifadhi na matumizi sahihi ya mazao yatokanayo na sekta hizo.

Awali akizungumzia namna maonesho hayo yalivyofanyika, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Dkt. Batilda Buriani amesema kuwa kupitia Maonesho ya mwaka huu wananchi wa mkoa huo wamepata fursa ya kujua teknolojia mbalimbali za Kilimo na Mifugo na Uvuvi na uzalishaji wa mazao yatokanayo na sekta hizo huku pia akibainisha kuwa maonesho hayo yalikuwa chachu ya kuhamasisha unywaji wa maziwa hasa kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari.

Maadhimisho hayo ya 45 tangu kuasisiwa kwake 1981 yalijumuisha taribani waoneshaji 578 na wajasiamali zaidi ya 70 waliofanikiwa kutoa elimu na kufanya biashara ya bidhaa mbalimbali zitokanazo na sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo