Kuhusu Sekta ya Uvuvi

Tanzania imebahatika kuwa na maeneo mengi ya maji baridi na maji ya bahari yenye rasilimali nyingi za uvuvi ambambo shughuli za uvuvi hufanyika. Tanzania Bara ina Ukanda wa Pwani wenye urefu wa kilometa 1,424 na upana wa maili za majini (nautical miles) 200. Eneo hilo la Bahari limegawanyika katika Maji ya Kitaifa (Territorial Sea) yenye upana wa maili za majini 12 sawa na kilometa za mraba zipatazo 64,000 na eneo la Bahari Kuu (Deep Sea) lenye upana wa maili za majini 188 sawa na kilometa za mraba zipatazo 223,000.

Eneo la maji baridi lina ukubwa wa kilometa za mraba 61,500 sawa na asilimia 6.5 ya eneo lote. Eneo hili linajumuisha maziwa makuu matatu ambayo ni Ziwa Victoria lenye kilometa za mraba 68,800 ambapo Tanzania inamiliki asilimia 51 sawa na kilometa za mraba 35,088; Ziwa Tanganyika lenye kilometa za mraba 32,900 ambapo Tanzania inamiliki asilimia 41 sawa na kilometa za mraba 13,489 na Ziwa Nyasa lenye kilometa za mraba 30,800 na Tanzania inamiliki asilimia 18.51 sawa na kilometa za mraba 5,700.

Aidha, kuna Maziwa Madogo 25 ambayo ni; Rukwa, Manyara, Eyasi, Babati, Kitangiri, Jipe, Chala, Ikimba, Singidani, Momela, Nguruka, Kindai, Natron, Basuto, Rwakajunju, Ambussel, Balangida, Burigi, Ngozi, Magadi, Lwelo, Hombolo, Merure na Ngoma.Pia kuna, Mabwawa ya Mtera na Nyumba ya Mungu na mito mikubwa 15 ambayo ni; Rufiji, Ruvuma, Wami, Pangani, Ruvu, Kagera, Malagarasi, Ruaha, Kilombero, Mara, Lukuledi, Matandu, Mbwemkuru, Umba na Songwe na maeneo oevu ya Malagarasi, Bahi nk

Sekta ya Uvuvi inayo fursa kubwa katika kuchangia kuondoa umaskini kwa kuwapatia wananchi ajira, kipato na chakula na lishe.Katika mwaka 2019, Sekta ya Uvuvi imetoa ajira ya moja kwa moja kwa wavuvi wapatao 202,053 na zaidi yawananachi milioni 4 wameendelea kutegemea shughuli mbalimbali zinazohusiana na Sekta ya Uvuvi zikiwemo uvuvi, biashara ya samaki, uchakataji wa samaki na mazao ya uvuvi na utengenezaji wa zana na vyombo vya uvuvi. Sekta ya Uvuvi inachangia asilimia 1.71 ya Pato la Taifa (Hali ya Uchumi 2019)

.