MRADI WA UZALISHAJI MBEGU BORA ZA MIFUGO MBIONI KUTEKELEZWA NCHINI
Nchi ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine na timu ya Watafiti kutoka chuo kikuu cha Jeonbuk nchini Korea inatarajia kutekeleza mradi wa utafiti na uzalishaji wa ng’ombe wa Maziwa kwa kutumia teknolojia za Uhimilishaji na Uhawilishaji wa viini tete.
Hayo yamebainishwa na Ujumbe wa Wawakilishi kutoka chuo kikuu cha Jeonbuk nchini Korea Prof. Hakkyo Lee, Mwondha Faluku na Rais wa Taasisi ya CACOON Bw. HeeJae ulioongozwa na Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya ambao walifika ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Agness Meena kwa ajili ya kutambulisha azma ya utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo, Bi. Meena amewataka wataalam hao kukaa pamoja na wataalam wa Wizara yake na kuwashirikisha wadau wengine wanaohusika na utekelezaji wa miradi nchini ili kujadili hatua sahihi za kufuata kabla ya utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa kuwa ndo mpo kwenye hatua ya usanifu wa mradi ni vema wataalam wetu wakashiriki kikamilifu ili kuona ni maeneo gani tunahitaji kunifaika zaidi kupitia mradi huo” Amesema Bi. Meena.
Kwa upande Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Prof. George Msalya ameeleza kuwa mradi huo utasaidia wafugaji nchini kupata mbegu bora za Ng’ombe wa maziwa hatua ambayo itaongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa nchini na kuhamasisha ufugaji unaotunza mazingira.