Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
WATENDAJI WANAOIHUJUMU SEKTA YA MIFUGO KUCHUKULIWA HATUA
.jpeg)
Baraza la Veterinari nchini limetakiwa kuwachukulia hatua kali watendaji na wataalamu wa sekta ya mifugo wanaofanya hujuma kwa wafugaji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina wakati akizindua Baraza la Veterinari (VCT), Bodi ya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo (LITA) na Bodi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) jijini Dodoma jana.
Waziri Mpina amesema kuwa kumekuwepo na tabia ya kukamata ng’ombe bila kuwapatia huduma muhimu ikiwemo maji na malisho hali inayosababisha mifugo mingi kufa huku mingine ikiuzwa kiholela na kusababisha hasara kwa wafugaji.
Pia alisema kuwa haiwezekani mifugo inakufa kwa siku moja halafu mfugaji anapewa cheti cha kifo wakati Wizara haijui mifugo imekufa na nini.
“Mifugo 942 imekufa kwa siku moja halafu mfugaji anapewa cheti cha kifo, Wizara haijui mifugo imekufaje, jambo hili ni hujma na Baraza la Veterinari mhakikishe mnalishughulikia hili na wahusika wachukuliwe hatua”, alisema Waziri Mpina
Katika hatua nyingine, Waziri Mpina amelitaka baraza hilo kuchukua hatua kali watu wa wasiokuwa watalaam wa magonjwa ya mifugo “vishoka” ambao wanajihusisha na utoaji tiba.
“Ni marufuku kwa vishoka kutoa huduma ya afya ya wanyama, na tukikutana nae, sio kosa tu la kulipa faini, bali itabidi twende kwenye fidia ambapo atalipa fidia kwa hasara aliyosababisha kwa mfugaji”, alisisitiza Waziri Mpina.
Aidha, Waziri Mpina amelitaka baraza hilo kuhakikisha katika mapendekezo ya maboresho ya sheria ya baraza wahakikishe suala la udhibiti wa vishoka linawekwa. Pia ameagiza wanachi waendelee kupewa elimu ili waweze kuwatambua vishoka. Vilevile Waziri Mpina ameliagiza baraza kuwafutia usajili na kuwazuia madaktaria wa mifugo ambao hawajahuisha taarifa zao kwenye daftari la usajili na kuhakikisha hawajihusishi na utoaji wa huduma.
Awali Waziri Mpina alitoa rai kwa bodi ya Uhifadhi wa Rasilimali za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kutangaza shughuli wanazofanya Pamoja na vivutio vilivyopo katika bahari na maziwa ili kuvutia shughuli za kitalii na kuongeza mapato.
Pia ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaweka mkakati na kuweka alama za mipaka yakiwemo maboya katika maeneo tengefu ili kuepuka migogoro na wananchi.
"Bodi ikaweke mipaka inayotambulika kama maboya katika Maeneo Tengefu na sio kukamata ovyo wavuvi na kusema wako ndani ya eneo la hifadhi wakati mipaka hakuna, hii itasaidia kupunguza migogoro”, alisisitiza Waziri Mpina.
Kwa upande wa Bodi ya LITA, Waziri Mpina ameitaka bodi hiyo kwenda kushughulikia changamoto zilizopo ikiwemo ya upungufu na ubovu wa miudombinu kama maabara, mabweni, maktaba na nyumba za walimu. Pia bodi hii imetakiwa kuhakikisha kuwa kuanzia Septemba – Octoba wafugaji 1500 wanapatiwa elimu ya ufugaji bora kwa kuingizwa darasani katika maeneo mbalimbali ya nchi.