Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
WALIOWAUZIA WAFUGAJI NG'OMBE WASIO NA SIFA WASAKWA

Serikali imeagiza kutafutwa kwa watu waliohusika kuwauzia kwa njia ya mkopo wafugaji ng’ombe wa maziwa waliozaa tayari na kuwahadaa wafugaji kuwa ng’ombe hao hawana uzao wowote (mitamba) ili wawapatie wafugaji ng’ombe wenye sifa kama walivyokubaliana katika mikataba.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, wakati akikabidhi lori moja la kukusanyia maziwa, keni za maziwa 250 pamoja na vifaa vingine vya kuboresha vituo vya kukusanyia maziwa kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU).
Pia alifafanua kuwa serikali imefanya kazi nzuri kuhakikisha wafugaji wanapata mikopo hiyo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), hivyo lazima ihakikishe wafugaji hao wananufaika.
“TDCU pamoja na vyama vya msingi hakikisheni wale waliowazuia ng’ombe wafugaji hawa wanafanya maboresho ili lengo la serikali liweze kukamilika, najua mmeuziana baina yenu lakini hatuwezi kama serikali kukaa kimya. Lengo letu ni kuhakikisha mkopo uliotolewa unaleta matokeo yaliyokusudiwa”, alisema Mhe. Ulega.
Naibu Waziri Ulega amesema kuwa endapo wafugaji hao wataendelea kuwa na ng’ombe hao watazidi kuwa masikini kwa kuwa watatumia nguvu kubwa kuwapatia malisho na dawa za mifugo ilhali ng’ombe hao wanatoa lita chache za maziwa tofauti na matarajio.
Aidha, wafugaji wa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa mkoani Tanga wametakiwa kuwa waaminifu kwa kuhakikisha wanapeleka maziwa ya yaliyo bora na yakutosha TDCU ili maziwa hayo yaweze kutosheleza mahitaji ya kiwanda cha kuchakata maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinapokea maziwa kupitia chama hicho.
Kuhusu bima ya mifugo, Naibu Waziri Ulega amesema kuwa Wizara kupitia Dawati la Sekta Binafsi imefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambapo tayari sera ya bima ya mifugo ipo tayari na kwamba ipo katika hatua ya mwisho. Sera hii itazinduliwa mwaka huu ili ianze kutumika na kuwanufaisha wafugaji pindi wanapopata majanga mbalimbali ya mifugo yao.
Naye Mratibu wa Miradi wa Usindikaji wa Maziwa Tanzania kutoka shirika la kimataifa la Heifer, Bw. Mark Tsoxo amesema mradi umewezesha upatikanaji wa loro la kukusanyia maziwa lenye thamani ya Zaidi ya shilingi milioni 170, matenki 6 ya kuhifadhia maziwa yenye ujazo wa lita 24,000, kukarabati vituo 10, jenereta 7 na malori 5 ya kubeba maziwa.
Bw. Tsoxo aalisema kuwa kutokana na jitihada za mradi kwa kushirikiana na wasindikaji, ukusanyaji wa maziwa umeongezeka kwa zaidi ya lita 12,000 kwa siku kutoka mwezi Januari lita 55,817 kwa siku hadi sasa lita 68,017 kwa siku.
Wafugaji waliopatiwa mikopo ya ng’ombe wa maziwa pamoja na ujenzi wa mabanda, wameishukuru serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa mkopo huo kutoka TADB na kuziomba taasisi nyingine kusaidia kuboresha zaidi mazingira ya ufugaji hapa nchini.
Vilevile wafugaji wameomba wataalam wa mifugo hapa nchini kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji juu ya ufugaji bora na wakibiashara na kuhakikisha wanawatembelea wafugaji mara kwa mara ili kuona maendeleo yao katika ufugaji.