WAKAGUZI MIFUGO,MAZAO YAKE WAPIGWA MSASA

Imewekwa: Wednesday 22, May 2024

WAKAGUZI MIFUGO,MAZAO YAKE WAPIGWA MSASA

◼️ Dkt. Lutege awapa somo la weledi na uadilifu

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi leo Mei 22, 2024 imeanza kutoa mafunzo ya siku 3 kwa Wakaguzi wa mifugo na mazao yake waliopo kwenye vituo mbalimbali vya ukaguzi ikiwa ni pamoja na vile vilivyopo kwenye mipaka yote nchini zoezi litakalofanyika mkoani Morogoro.

Akifungua Mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Dkt. Benezeth Lutege amewataka wataalam hao mbali na kutumia vema taaluma zao, wazingatie weledi na watende haki wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuomba ushauri pale wanapopata changamoto.

“Tunapokuwa kule kwenye vituo vyetu vya ukaguzi tunapaswa kujua sisi ndio sura ya Wizara kwa hiyo tunavyowapokea wageni, tunavyoongea nao na tunavyotoa huduma zetu kuna athari kubwa sana kwa viongozi wetu wanaotusimamia hivyo tunaweza kuwachafua au kuwajengea sifa njema” Ameongeza Dkt. Lutege.

Aidha Dkt. Lutege ametoa angalizo kwa vijana hao kuacha kutanguliza mbele maslahi yao wakati wakitekeleza majukumu vituoni ili kuendelea kujenga dhana ya uaminifu na uadilifu jambo litakalolinda taswira ya Wizara na Serikali kwa ujumla.

“Akifika Mteja umemkamata, unatakiwa kumueleza makossa yake kwa moyo mweupe kabisa na kwa lugha stahiki bila kutumia nguvu au lugha chafu kisha na yeye umpe nafasi akueleze sababu zake na baada ya hapo upime kwa taaluma yako uone kama alichofanya ni kosa la kukusudia au la ndipo ufanye maamuzi” Amesisitiza Dkt. Lutege.

Kwa Upande wake Mratibu wa Mradi wa Mfumo wa Usalama wa Wanyama, Mimea na Chakula ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Baltazar Kibola amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wataalam hao kufahamu kuhusu Afya ya wanyama na mazao yake kabla hawajatoa vibali kupitia mfumo wa utoaji vibali vya Mifugo na Mzao yake kielektroniki (MIMIS).

Naye Mratibu wa Mradi huo kutoka Shirika la “TradeMark Africa” ambao ndio wafadhili wakuu wa Mafunzo hayo Bi. Kezia Mbwambo ameeleza kuwa Shirika lake liliona umuhimu wa wataalam hao kujengewa uwezo kuhusu masuala ya usalama wa mifugo na mazao yake ili kulinda afya za Mifugo na watumiaji wa mifugo hiyo kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya wataalam wenzake, Afisa Mfawidhi wa kituo cha Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake Wilaya ya Temeke Bi. Mwajuma Chaurembo amelishukuru Shirika hilo kwa kuwajengea uwezo kupitia mafunzo hayo ambapo ameahidi kufanyia kazi kwa vitendo yote watakayojifunza kwa siku zote tatu.

Mafunzo hayo yanafuatia mafunzo ya awali yaliyodhaminiwa na Shirika la “TradeMark Afrika” na kuratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kitego chake cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano ambayo yalihusu mfumo wa utoaji wa Vibali vya Mifugo na Mazao yake kielektroniki (MIMIS).

.