​WAFUGAJI WAKIJENGEWA UWEZO WATAKUZA UCHUMI WA TAIFA - MONGELA

Imewekwa: Friday 13, November 2020

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongela amesifu juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha wafugaji wake wanafanya shughuli hiyo kwa tija na kwa kuzingatia dhana ya ukuzaji wa uchumi wao.

Mhe. Mongela ameyasema hayo leo (12.11.2020) baada ya kupokea timu ya wataalam wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo (Wizara ya Mifugo na Uvuvi) ambao wamefika mkoani humo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya siku mbili kwa wakaguzi wa vyakula vya mifugo kuhusu ukaguzi wa maeneo ya malisho na rasilimali za vyakula vya Mifugo

"Tunajitahidi sana kukuza tasnia ya ufugaji lakini uwepo mafunzo kama haya unawafanya wafugaji wetu wasiishie tu kufuga bali wafuge kwa tija na kukuza uchumi wao" amesema Mhe. Mongela.

Mhe. Mongela ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea na jitihada hizo za kujenga uwezo kwa wafugaji ili kuwafanya kuwa wafugaji bora wenye uelewa na ujuzi wa ufugaji wa kisasa badala ya ufugaji wa asili ambao haukuwa na tija kwa mfugaji pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mifugo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza amesema kuwa wakaguzi hao ni sehemu ya wakaguzi 129 walioteuliwa kutoka kwenye Halmashauri na Sekretarieti za mikoa hapa nchini ambao baada ya kupatiwa mafunzo hayo watawawezesha wafugaji waliopo kwenye maeneo yao elimu kuhusu chakula bora cha mifugo ili waweze kuiboresha na kuongeza tija zaidi kwenye tasnia hiyo.

"Semina hii ni muhimu sana hivyo ninaomba tushirikiane na kwa sababu ninafahamu kuwa wote mna ujuzi hivyo leo tupo hapa kwa ajili ya kuongezeana uwezo wa kuwahudumia vizuri wafugaji wetu hasa ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 70 ya mahitaji ya mfugo ni chakula" Ameongeza Dkt. Rwiguza

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel ni ya awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza ilifanyika mkoani Morogoro na kuhusisha Mikoa ya Dar-es-Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga na Dodoma.

.