WAFUGAJI WAHIMIZWA KUPANDA MALISHO YA MIFUGO

Imewekwa: Tuesday 15, April 2025

Na. Stanley Brayton, WMUV - Dodoma

◼️Waelezewa athari za kulisha Mifugo katika maeneo ya Hifadhi za Misitu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ndg. Abdul Mhinte, amewataka wafugaji Wilayani Bahi na Chamwino kupanda Malisho kwa ajili ya Mifugo ili kuepukana na changamoto za kukosa Malisho ya Mifugo.

Akizungumza katika Kikao na Wafugaji cha kujadili changamoto zao na kuzitafutia Ufumbuzi, kilichofanyika leo Aprili 15, 2025, Mkoani Dodoma, katika Kitongoji cha Mtungutu, Kata ya Zanka, Kijiji cha Mayamaya, Wilaya ni Bahi, Ndg. Mhinte, amesema yapo maeneo muhimu ya Malisho ambayo yametengwa na Serikali ili kutatua changamoto za Malisho.

"yapo maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya Malisho japo yanapungua kadri Mifugo inavyozidi kuongezeka, na ni muhimu kuhakikisha kila mfugaji anapanda Malisho kwa ajili ya Mifugo yake" amesema Ndg. Mhite

Vilevile, Ndg. Mhite amebainisha kuwa maeneo ya Malisho yanapungua kadri Mifugo na watu wanavyoongezeka, kiasi cha kwamba kunapelekea Misitu na Malisho kupungua au kutoweka kabisa.

Pia, Ndg. Mhinte ametolea ufafanuzi kuhusu athari za kulisha Mifugo katika maeneo ya Hifadhi ya Misitu, ikiwa ni pamoja na kuharibu Hifadhi hiyo na hatimaye kuamia katika Hifadhi zingine na kuziharibu na mwishowe kukosa Malisho kabisa pamoja na kuharibu Hifadhi hizo.

Ndg. Mhinte amesema kuwa Biashara ya kupanda Malisho imekuwa kama Dhahabu na hii ndio itakayosaidia wafugaji wengi katika kulisha Mifugo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za vyakula za Mifugo. Dkt. Asimwe Rwiguza, amesema kwa sasa Serikali haitegemei Malisho ya asili kwa sababu haitoshelezi idadi ya Mifugo ambayo tunayo hapa nchini.

Dkt. Rwiguza amefafanua kuwa kwa sasa kuna namna ya kukabiliana na changamoto za Malisho, ikiwa ni pamoja na kulima Malisho, na ndio maana Serikali imetoa maeneo maalum kwa ajili ya kupanda Malisho na inaendelea kutoa mbegu hizo za Malisho na kutoa elimu namna ya kupanda hizo mbegu ili kuhakikisha kila mfugaji anakuwa nazo na anapandikiza katika eneo lake.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wote, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Bw. Kusundwa Wamalwa amesema zipo changamoto nyingi zinazowakumba wafugaji wengi hususan wa hapa Wilaya ya Bahi na Chamwino, ikiwemo Maji, Malisho na Masoko, kwa hiyo ni vyema Serikali ikaangalia ni jinsi gani itaweza kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji hao

Naye, Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Bw. Mathew Kiondo amesema miaka ya nyuma TFS ilitoa Hekta 2000 kwa wafugaji, ila kutokana na ongezeko la watu limepelekea Mahitaji ya Malisho kuwa makubwa kutokana na idadi kubwa ya watu na Mifugo, kwa hiyo wao kama TFS wataangalia ni jinsi gani wataweza kufanya ili kunasua wafugaji na changamoto ya uhaba wa maji kupitia Mfuko wa Kusaidia Jamii (CSR), ili kuwatengenezea Miundombinu ya maji kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Chenene kwenda kwenye maeneo yao ya Ufugaji.

.