UANDAJI WA MITAALA YA MAFUNZO YA MIFUGO USHIRIKISHE WADAU WA KISEKTA – MHINTE

Imewekwa: Monday 10, February 2025

UANDAJI WA MITAALA YA MAFUNZO YA MIFUGO USHIRIKISHE WADAU WA KISEKTA – MHINTE

Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Abdul Mhinte amesema uandaaji wa mitaala kwaajili ya mafunzo ya mifugo kwa vyuo vya kati ushirikishe wadau wa sekta husika pamoja kuzingatia sera mpya ya elimu na mafunzo mwaka 2014 Toleo la 2023 ili kupata mahitaji halisi yanayohitajika kwenye soko la sasa.

Naibu Katibu Mkuu Mhinte amesema hayo leo Februari 7, 2025 mkoani Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha kufanya mapitio ya rasimu ya mitaala iliyoandaliwa ya mafunzo ya mifugo kwa vyuo vya kati na kutoa wito kwa timu ya wataalam inayoandaa mitaala hiyo kuhakikisha mitaala mipya inayoandaliwa inaendana na sera ya elimu na mafunzo iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.

“Mitaala hii ya kisekta inapoandaliwa inatakiwa kufanyika kwa kushirikisha wadau wa ile sekta, kwasababu usipofanya hivyo unaweza kuandaa mitaala ambayo ikifika kwenye matumizi washiriki au watumiaji wake wanaweza kuona mitaala hiyo haijawasaidia, sasa wakati tunatoa maoni ya kuandaa mitaala hii ni muhimu tuzingatie sera yetu mpya ya elimu ” alisema Mhinte.

Aidha Mhinte ameongeza kwa kusisitiza kuwa mitaala mipya ya mafunzo ya mifugo inayoandaliwa izingatie mabadiliko ya hali ya teknolojia, mambo mbalimbali yanayotokea duniani katika nyanja ya masoko, biashara na uzalishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya mafunzo, utafiti na huduma za ugani Dk. Angello Mwilawa amesema maboresho ya mitaala inayotumika kwaajili ya mafunzo ya mifugo kwa vyuo vya kati hufanyika kila mara baada ya miaka mitano lengo ikiwa ni kuangalia hali ya halisi ya masomo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la sasa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa wakala wa Mafunzo ya vyuo vya mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema pamoja na mambo mengine rasimu ya mtaala ianyoaandaliwa imezingatia sera ya mifugo ya mwaka 2006 pamoja na mikakati ya mabadiliko ya sekta ya mifugo ikiwemo program ya jenga kesho iliyobora BBT.

.