TUPAZE SAUTI KUOKOA PUNDA-MNYETI

Imewekwa: Friday 17, May 2024

TUPAZE SAUTI KUOKOA PUNDA-MNYETI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka wadau wote wanaosimamia ustawi na haki za wanyama kukemea vikali vitendo vitakavyosababisha kutoweka kwa Punda ili wanyama hao waendelee kuwasaidia wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mhe. Mnyeti ametoa rai hiyo Mei 17, 2024 alipokuwa akifunga Maadhimisho ya siku ya Punda Afrika Mashariki ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma yakitanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo mijadala iliyolenga kuchukua hatua mbalimbali za kunusuru kutoweka kwa mnyama huyo.

“Punda wamekuwa wakifanya kazi kubwa na muhimu sana katika sekta za kiuchumi ambapo katika shughuli za usafiri hivi sasa wamekuwa wakitumika mpaka kubeba vifaa vya ujenzi na siku za hivi karibuni tumeshuhudia wakibeba madini katika migodi mbalimbali nchini” Ameongeza Mhe. Mnyeti.

Aidha Mhe. Mnyeti amebainisha kuwa kutokana na umuhimu wa ngozi na viungo vingine vya mnyama huyo ongezeko la uchinjaji wa wanyama hao lilikuwa kubwa hali iliyosababisha tishio la kutoweka kwao Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

“Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kudhibiti kutoweka kwa wanyama hawa ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli za uchinjaji wake na biashara ya ngozi zake zilizokuwa zikiendeshwa kwa leseni ya muda ya kampuni ya Fan-Hu kutoka China na kama tungekiacha kiwanda hiki kiendelee kufanya kazi kwa miaka miwili basi kusingekuwa na punda hata mmoja hapa nchini” Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Kwa upande wake Mtaalam wa Mifugo na mmoja wa watetezi wa haki za Punda Dkt. Bedarn Masuruli ameipongeza Serikali kwa hatua zake mbalimbali za kuhakikisha mnyama huyo hatoweki huku pia akitoa rai kwa Serikali kuwazingatia wanyama hao katika Sera na Mipango inayohusiana na Mifugo.

“Wadau wamepongeza hatua ya Serikali kuungana na Taasisi zilizo chini ya Umoja wa Afrika kuandaa mkutano wa kwanza wa Afrika kuhusu Punda uliozaa azimio la Dar Es Salaam ambalo linasema “Punda Afrika Sasa na katika Siku zijazo” Amesema Dkt. Masuruli.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Anette Kitambi ameitaka jamii kushirikiana na Serikali kuwalinda Punda kwani mfumo wa uzazi ni tofauti na wanyama wengine ambapo anaweza kuzaa mara moja au asizae kabisa na muda wake wa kubeba mimba huwa ni kati ya miezi 12 hadi 14.

“Na maajabu mengine ya punda kama akiona mazingira sio rafiki anaweza kuahirisha kuzaa hivyo ni mnyama mwenye sifa za tofauti kabisa ukiinganisha na wengine na ndio maana kutokana na umuhimu huo kati ya wanyama wote ni yeye tu ndo aliandaliwa siku yake kitaifa” Amebainisha Dkt. Kitambi.

Maadhimisho ya Siku ya Punda duniani hufanyika Mei 08 ya kila mwaka na kwa Afrika Mashariki huwa ni Mei 17 huku Serikali, wataalam na wadau mbalimbali wakitumia siku hiyo kujadili hatma ya mnyama huyo na ustawi wake kwa ujumla.

.