TANZANIA YAPOKEA DOZI 1000 ZA MBEGU ZA NG'OMBE BORA WA NYAMA KUTOKA INDONESIA

Imewekwa: Monday 02, December 2024

TANZANIA YAPOKEA DOZI 1000 ZA MBEGU ZA NG'OMBE BORA WA NYAMA KUTOKA INDONESIA.

Ni za Ng'ombe wa kuanzia kilo 700

Nchi ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji wa Mifugo (NAIC) kilichopo mkoani Arusha leo Desemba 02, 2024 imepokea dozi 1000 za mbegu za Ng'ombe bora wa nyama kutoka nchini Indonesia ambazo zitawawezesha wafugaji nchini kuongeza kiwango cha uzalishaji wa zao la nyama.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Mifugo Bw. Stephen Michael mbali na kuishukuru Serikali ya Indonesia kwa msaada huo amebainisha kuwa mbegu hizo zitakuwa chachu ya ubora wa Mifugo inayozalishwa nchini.

"Kuna mbegu aina ya Lemousine ambayo Ng'ombe wake anaweza kufikia hadi kilo 900 hivyo badala ya kufuga ng'ombe 4 wa kilo 200 mfugaji anaweza kuwa na ng'ombe huyo mmoja tu ambapo pia itamsaidia kupunguza gharama za ufugaji kwa upande wa chakula na matibabu" Amesema Bw. Michael.

Akieleza dhumuni la kutoa mbegu hizo Mtaalam kutoka Wizara ya Kilimo nchini Indonesia Bi. Arsdiana Devi amesema kuwa msaada huo ni matokeo ya mafunzo ya awali baina ya wataalam kutoka Wizara yake na wale wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi zake ambapo walisaini makubaliano ya ushirikiano katika kukuza sekta ya Mifugo baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini (CWT) Bw. Murida Mshota amesema kuwa ujio wa mbegu hizo unawafanya Wafugaji waingie kwenye mfumo mpya wa ufugaji ambapo baada ya kupandikiza mbegu hizo wataondokana na ufugaji wa ng'ombe wenye uzito mdogo ambao hawakuwa na tija wanayoitarajia.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Ng'ombe kibiashara Bw. Peter Makang'a ameishukuru Serikali ya Indonesia kwa kuona umuhimu wa kuboresha mbegu za Mifugo nchini huku akiongeza kuwa chama chake kitafikisha mbegu hizo kwa wafugaji ambao hawakubahatika kupata mbegu bora hapo awali.

Dozi hizo 1000 za mbegu zitatolewa kwa wadau wa Ufugaji nchini ambapo Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) itapata dozi 500, Chama cha Wafugaji nchini dozi 200 Chama cha Wafugaji kibiashara kitapata dozi 100, Wadau wa Bodi ya Nyama watapata dozi 200 na Wadau wengine wa Ufugaji dozi 200.

.