Tanzania na Uganda za Saini Makubaliano ya Kuboresha Sekta ya Mifugo

Imewekwa: Monday 15, January 2018

TANZANIA NA UGANDA ZASAINI MAKUBALIANO YA KUBORESHA SEKTA YA MIFUGO
Na John Mapepele
Tanzania na Uganda leo zimesaini makubaliano ya kuboresha sekta ya mifugo baina ya nchi mbili kwa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kuthibiti magonjwa hatari ya mlipuko na kuanzisha minada ya pamoja ya kimataifa kwa maslahi ya nchi zote mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa kwa upande wa Uganda na Balozi wa Uganda nchini bwana Richard Tumusiime Kabonero na kwa upande wa Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo mjini Bukoba.
Akizungumza mara baada ya utiaji wa saini makubaliano hayo Balozi Kabonero amesema magonjwa ya mlipuko kwa wanyama hayana mipaka hivyo makubaliano yaliyofanyika yatasaidia kudhibiti magonjwa ya wanyama hatimaye kuboresha mifugo.
Aidha, amesema hatua ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo itasaidia kupata mifugo bora itakayokuwa na thamani kubwa katika masoko ya kimataifa na kuingizia nchi zote mbili mapato zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo nchi zinapata hasara kwa kuuza mifugo ikiwa katika kiwango cha chini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo amesisitiza kwamba ushirikiano wa kitaalam katika kuratibu,kufuatilia hali ya mifugo na kufanya tathmini ya kila wakati utaleta mafanikio makubwa baina ya nchi ya Tanzania na Uganda utaleta mapinduzi katika sekta badala ya utaratibu wa sasa wa kila nchi kushughulikia masuala ya peke yake.
“Magonjwa ya mlipuko kwa wanyama ni suala mtambuka duniani kote, hivyo ni muhimu kulishughulikia kwa pamoja ili kuwa na tija” alisisitiza Dkt. Mashingo.

.