Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
TAFITI ZILENGE KUONGEZA UZALISHAJI NA SIO WINGI WA MIFUGO-PROF. SHEMDOE.

TAFITI ZILENGE KUONGEZA UZALISHAJI NA SIO WINGI WA MIFUGO-PROF. SHEMDOE.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewataka watafiti wanaojihusisha na sekta ya Mifugo kuhakikisha tafiti zao zinalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo badala ya wingi wa Mifugo ili kuwawezesha wafugaji waliopo nchini kujikita kwenye uzalishaji wenye tija.
Prof. Shemdoe ameyasema hayo kwenye warsha ya kufunga mradi wa utafiti wa Unenepeshaji wa ng'ombe iliyofanyika Disemba 18,2023 makao makuu ya wizara hiyo yaliyopo Mtumba jijini Dodoma.
"Sipati furaha sana kusikia tuna mifugo Mil.36.6 kwa sababu kwangu mimi hiyo haina thamani, shauku yangu ni kuona tuna kiasi gani cha nyama bora, uzito wa mifugo yetu umeongezeka na sio wingi wa mifugo ambayo haina mchango kwenye ongezeko la uzalishaji na uuzaji wa mazao ya mifugo ikiwemo nyama kwenye soko la ndani na nje ya nchi hivyo ni lazima tafiti zetu ziangalie namna ya kufanikisha hilo" Ameongeza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa ongezeko la mifugo isiyo na tija linasababisha kuendelea kwa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi kutokana na ukweli kuwa eneo la kukidhi ongezeko la mifugo hiyo lipo vile vile hivyo amewataka wafugaji kuongeza mifugo yenye tija ili wavune na kupata faida na kuongeza pato lao na Taifa kwa ujumla.
"Soko la nje kwa sasa halihitaji ng'ombe mwenye zaidi ya miaka 3 lakini ukiangalia karibu asilimia 90 ya ng'ombe hawa wengi tulionao hapa nchini inawezekana wana umri wa zaidi ya miaka hiyo" Ameongeza Prof. Shemdoe.
Akiwasilisha taarifa hiyo ya Mradi wa Utafiti, Mratibu Mkuu wa mradi huo Prof. Ismail Selemani amesema kuwa lengo la mradi huo lilikuwa ni kutafuta vyakula vya bei nafuu ambavyo vitatumika kwa ajili ya unenepeshaji wa ng'ombe wa asili ili kuongeza uzalishaji wa nyama bora itakayouzwa katika soko la ndani na lile la kimataifa.
"Tafiti za nyuma zimeonesha nchi yetu ina ng'ombe wengi wa asili ingawa changamoto kubwa imekuwa ni uzalishaji duni wa mazao ya nyama na changamoto kubwa inayosababisha hali hiyo ni chakula cha kunenepeshea mifugo hiyo hivyo baada ya utafiti tumegundua chakula kinachochanganywa na mazao ya mihogo kinafanya vizuri zaidi kwenye unenepeshaji" Ameongeza Prof. Selemani.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Bw. Ntufye Mwakinonja amesema kuwa mradi huo umetekelezwa chini ya ufadhili wa Taasisi hiyo kupitia mfuko wake wa kuendeleza Sayansi na Teknolojia ambapo ulitenga takribani shilingi milioni 240 ya kugharamia miradi ya unenepeshaji wa Mifugo kwenye Taasisi ya utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichotekeleza mradi huo.
Naye mmoja wa wafugaji walioshiriki warsha hiyo kutoka wilayani Kongwa Bi. Juliana mahava ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha matokeo ya tafiti hizo ambazo zinalenga kuboresha shughuli zao za ufugaji.
"Tulikuwa tunafuga ng'ombe kwa mtindo wa kuchunga kwa miaka zaidi ya minne bila kupata tija lakini kupitia utafiti huu tunaona sasa kuwa tunaweza kuwa na mifugo michache na kuinenepesha kwa siku 75 tu na kupata faida kubwa zaidi" Ameongeza Bi. Mahava.
Mradi huo wa Utafiti wa unenepeshaji wa ng'ome wa asili umetekelezwa kwa miaka 2 na umefadhiliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Utafiti ya Canada ambayo hugharamia tafiti mbalimbali za shughuli za ugani.