Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
SERIKALI YAPANIA KUTOKOMEZA MAGONJWA 'SUMBUFU' KWA MIFUGO

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mkakati madhubuti wa kutokomeza Magonjwa yanayoandama mifugo ili kuwa na mifugo bora itakayozalisha kwa tija na kukuza uchumi wa nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Tanzania, Profesa Hezron Nonga katika Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari uliofanyika jijini Dodoma Juni 4,
2020.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, Profesa Nonga alisema kuwa Tanzania kuna mifugo takriban milioni 34 lakini pamoja na wingi huo wa mifugo bado nchi haijafikia uzalishaji mkubwa kutokana na magonjwa yanayoandama mifugo hiyo.
Kufuatia hali hiyo, alisema kuwa Mwaka 2018 Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliamua kuja na mkakati wa kufanya mageuzi makubwa katika huduma za mifugo upande wa afya ili kuwa na mifugo bora itakayotoa mazao bora na salama kwa matumizi ya binadamu.
Profesa Nonga alisema mkakati huo ambao umejikita zaidi katika kukinga mifugo dhidi ya magonjwa umeweka utaratibu wa kuhakikisha mifugo yote inaogeshwa na kupata chanjo stahiki dhidi ya magonjwa ya kipaumbele.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo magonjwa yanayochangia kukwamisha uzalishaji wenye tija kwa mifugo nchini ni ugonjwa wa miguu na midomo, Ndiganakali na mapele ngozi.
“Lengo letu ni kuhakikisha mifugo yote nchini inapata chanjo kulingana na kalenda ya uchanjaji ili kuwakinga na magonjwa hayo sumbufu”, alisema Profesa Nonga.
Aidha, alisema mkakati huo umepanga kuwa katika kila Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa kuwe na Majosho ya kuogeshea ng’ombe na mifugo mingine walau mara mbili kwa mwaka ili kuwalinda na maradhi yanayosababishwa na Kupe pamoja na wadudu wengine.
“Kwa mfano Kupe anachangia vifo vya Ng’ombe kwa zaidi ya asilimia 70, hivyo ni muhimu kuzuia magonjwa yanayosababishwa na wadudu hawa ili tuwe na ufugaji wenye tija zaidi nchini, maana ufugaji unakuwa hauna tija pale ambapo wanazaliwa Ndama kumi halafu wanakufa tisa unabaki na mmoja” alifafanua Mkurugenzi huyo.
Katika kuhakikisha suala la kuogesha mifugo linafanikiwa, alisema kwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 Serikali imeshajenga majosho 85 na kukarabati majosho 288 na kusisitiza hawataki kuona mifugo inaendelea kufa wakati wataalamu wapo.
Pia alisema mkakati huo umeweka utaratibu mzuri wa ununuzi wa pamoja wa chanjo (bulk procurement system) na zitasambazwa katika maeneo yote kuanzia ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya mkoa ili ziwe zinapatikana kwa urahisi.