SERIKALI KUTAFUTA SULUHISHO YA MIALO KUFURIKA MAJI ZIWA TANGANYIKA

Imewekwa: Sunday 31, March 2024

SERIKALI KUTAFUTA SULUHISHO YA MIALO KUFURIKA MAJI ZIWA TANGANYIKA

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutekeleza mkakati wa kutafuta suluhisho la kufurika kwa maji katika mialo ya ziwa Tanganyika leo machi 27, 2024 mkoni Kigoma.

Akizungumza na wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi, Katibu mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema serikali imeanza kufanya tathimini juu ya kufurika kwa maji kwa baadhi ya miundombinu ya mialo ya ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ambayo inatajwa kuchagizwa na mabadiliko ya Tabia nchi.

Prof. Shemdoe alitoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea baadhi ya mialo ikiwemo Kibirizi, Myobozi na Katonga ambayo baadhi ya miundombunu yake imefurika maji na kulazimu shughuli za biashara ya mazao ya uvuvi kusimama, na kusisitiza kuwa ofisi yake itashirikiana na Sekretarieti za Mikoa ili kuona namna nzuri ya kurejesha huduma kwa wakazi ambao tegemeo lao ni ziwa Tanganyika .

“Kama mnavyo ona kumekuwa na changamoto ya kufurika kwa mialo kutokana na kuongezeka kwa maji, hivyo tumekuja kuona ili sisi kama Wizara tuweze kukaa na wenzetu wa TAMISEMI kuona ni wapi tunawezeza kubadilisha na hasa haya masoko ambayo yamekwisha athirika na maji” alisema Prof .Shemdoe.

Prof. Shemdoe alisema maji hayo hayajaathiri tu masoko kwenye mialo bali hata chuo cha wakala wa elimu na mafunzo ya Uvuvi FETA kampasi ya Kigoma ambacho miundombinu yake imejaa maji na hivyo kulazimika kusitisha masomo kwa muda wa wiki mbili ili kutafutiwa eneo ambalo wataweza kuendelea na masomo yao huku serikali ikikamilisha mchakato wa kutafuta eneo zuri ambalo kampasi hiyo itajengwa upya.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara na wavuvi katika

Mialo ya Kibirizi, Muyobozi na Katonga wamesema hali ya kujaa maji katika maeneo ya mialo ya ziwa Tanganyika imeathiri pakubwa shughuli zao kwani baadhi ya miundombinu iliyokuwa ikitumika kwa sasa imefurika maji.

Naye, mfanyabiashara wa mazao ya uvuvi, Bi. Anastazia Nicholaus alisema kupungua na kujaa maji katika Ziwa Tanganyika ni hali ambayo imekuwa ikijitokeza kwa kipindi cha masika japo kwa kipindi hiki maji yameanza kufurika zaidi ikilinganishwa na vipindi vya nyuma.

“hali hii inatuathiri sana sisi wafanyabiashara kwa sababu shughuli zetu za uchakataji samaki zimesimama kutokana na vichanja vya kuchakatia samaki kujaa maji, hivyo basi tunaiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itusaidie sehemu nyingine kwa ajili ya kuchakatia samaki” alisema.

.