Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
SERIKALI KURASIMISHA BIASHARA YA MABONDOKURASIMISHA BIASHARA YA MABONDO

Serikali imesema itahakikisha inachukua hatua ya kuwepo kwa taratibu maalum zilizo wazi kwenye biashara ya mabondo ya samaki ili kujiridhisha upatikanaji wake hadi kufika viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.
Akizungumza leo (05.03.2024) jijini Mwanza na wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi katika jiji hilo, wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema serikali itahakikisha inaweka utaratibu ili kujiridhisha namna ya upatikanaji wa mabondo.
Prof. Sheikh amebainisha hayo baada ya baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi kulalamika kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakivua samaki ambao wako chini ya viwango vinavyotakiwa viwandani wakiwa na lengo la kuuza mabondo kwenye viwanda vya kuchakata mabondo hayo na kuharibu mazalia ya samaki.
Ameongeza kuwa lazima kuwepo utaratibu maalum kujua upatikanaji wa mabondo hadi kufika kwenye viwanda kwa ajili uchakataji ili samaki wanaovuliwa wawe ni wale ambao wana viwango vinavyotakiwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa.
Kuhusu uvuvi wa dagaa kwa kutumia taa za solar na zana zingine za uvuvi ambapo inaelezwa wavuvi wamekuwa wakivua hadi dagaa ambao wanatakiwa kuwa chakula cha samaki aina ya sangara, Prof. Sheikh amesema serikali itaendelea kufanya taifiti zaidi kwa kuishirikisha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ili kuwa na matokeo sahihi.
Amesema kuwa serikali kupitia TAFIRI ni lazima ifanye tafiti za kujiridhisha matokeo yaliyotolewa awali kama yana athari yoyote kabla ya kuwa na matokeo mengine na kuyatolea ufafanuzi ili kuwa na matokeo yasiyokuwa na utata.
Prof. Sheikh amewataka pia wafanyabiashara kuzidi kushirikiana na serikali katika juhudi za kukuza Sekta ya Uvuvi kwa kuunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kurasimisha sekta hiyo ili iwe endelevu.
Nao baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi jijini Mwanza, wameiomba serikali kupitia Wizara ya Uvuvi kuzidi kuchukua hatua katika kupambana na uvuvi haramu ili samaki wazidi kuzaliana kwa wingi na kuongeza wingi wa samaki katika viwanda.
Aidha, wamesema ni muhimu kulinda soko la nje katika kuuza mazao ya uvuvi ili kuliongezea taifa mapato zaidi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
Katika kikao hicho ambacho Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiwazungukia wadau mbalimbali wa Sekta ya Uvuvi kupata maoni yao ya namna ya kulinda rasilimali za uvuvi, imesema itakuwa inafanya vikao mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Kabla ya kikao hicho Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh alifika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa mkoa huo Bw. Balandya Elikana kuhusu hali ya Sekta ya Uvuvi Mkoani Mwanza ambapo aliarifiwa kuwa uongozi wa mkoa umekuwa ukihakikisha unalinda rasilimali za uvuvi ili ziwanufaishe wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla