SERIKALI KUJENGA UZIO SHAMBA LA MIFUGO MABUKI.

Imewekwa: Tuesday 12, March 2024

SERIKALI KUJENGA UZIO SHAMBA LA MIFUGO MABUKI.

◾ Ni mkakati wa kudhibiti uvamizi wa mifugo shambani hapo

Naibu waziri wa Mifugo na uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesikitishwa na taarifa za uvamizi wa makundi ya wafugaji kwenye Shamba la Mifugo la Mabuki lililopo mkoani Mwanza ambapo ameweka wazi mpango wa Serikali kuweka uzio unaozunguka shamba hilo ili kudhibiti tatizo hilo.

Mhe.Mnyeti amebainisha hayo leo Machi 12, 2024 wakati akizungumza na wanufaika wa programu ya "Jenga kesho iliyo bora kwa wajasiriamali wanawake na vijana (BBT-LIFE) waliopo kwenye shamba hilo ,mara baada ya kupewa taarifa ya uvamizi wa mara kwa mara wa makundi ya mifugo kutoka kwa wafugaji Kata za Misasi,Kijima,Mabuki na Kata za Wilaya za jirani.

"Wizara itaweka utaratibu wa kujenga uzio kuzunguka shamba hili na ujenzi huo utafanyika kwa awamu kuanzia maeneo ya Kata zenye uvamizi mkubwa ikiwemo Kata ya Kijima na Misasi ili kukabiliana na kukomesha uvamizi wa mifugo kwenye hifadhi ya shamba hili ambalo kimsingi ni rasilimali ya nchi siyo ya Misungwi pekee na ni muhimu likalindwa kwa manufaa ya wote" amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Mhe. Mnyeti ameongeza kuwa uzio huo utadhibiti mwingiliano wa mifugo ya Serikali na ile iliyopo chini ya programu ya "BBT-LIFE ili kuepusha mlipuko wa magonjwa ya mifugo yanayo tokana na mwingiliano wa makundi ya mifugo.

Mhe.Mnyeti ameeleza kwamba Serikali itatoa fedha za kujenga na kukarabati malambo ili kupata huduma ya maji na kuwataka wataalamu kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wafugaji ili waweze kufuga kisasa.

.