​SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI ZAPAA MKOANI KAGERA

Imewekwa: Sunday 13, October 2024

Sekta za Mifugo na Uvuvi zimeonekana kufanya vizuri ukilinganisha na sekta nyingine mkoani Kagera kutokana na ongezeko la kila mwaka kwenye uzalishaji wa mazao ya sekta hizo.

Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Dkt. Abel Nyamahanga katika hotuba yake ya ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani uliofanyika leo Oktoba 13, 2024 mkoani Kagera ambapo amesema kuwa ongezeko la uzalishaji wa nyama na maziwa limetokana na wafugaji wa mkoa huo kuhamasika kufuga kisasa huku wengi wakifuga kwenye ranchi ya Kikulula iliyopo Wilaya ya Misenyi mkoani humo.

“Uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita mil. 46 mwaka 2021 na kufikia lita mil. 71 mwaka huu (2024) wakati upande wa nyama uzalishaji kwa matumizi ya mkoa umefikia tani 5000 kwa mwaka huku takribani ng’ombe elfu 30 husafirishwa kwenda kwenye mkoa mingine kwa ajili ya kuchangia upatikanaji wa nyama kwenye mikoa hiyo na kwa hili hatuna budi kujipongeza kwa sababu tumepiga hatua kubwa” Ameongeza Dkt. Nyamahanga.

Aidha Dkt. Nyamahanga amesema kuwa mkoa huo umeendelea kufanya vizuri kwa upande wa uzalishaji mazao ya Uvuvi ambao amebainisha uzalishaji wa samaki umeongekeza kutoka tani 7266 kwa mwaka 2020 hadi tani 30935 kwa mwaka 2024 ambapo amesisitiza kuwa ongezeko hilo limetokana na jitihada za Serikali za kutoa elimu kuhusu Uvuvi salama na kudhibiti uvuvi haramu.

Kwa Upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Mary Yongolo amesema kuwa Wizara yake inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya 6 katika kuboresha sekta za Mifugo na Uvuvi ambapo amewataka wananchi wote hususan wafugaji na wavuvi kufika kwenye Maonesho hayo ili waweze kupata elimu ya ufugaji wa kisasa na Uvuvi salama.

.