SEKTA YA UVUVI YAPOKEA MAGARI, PIKIPIKI ZA MRADI WA AFDP

Imewekwa: Tuesday 12, March 2024

SEKTA YA UVUVI YAPOKEA MAGARI, PIKIPIKI ZA MRADI WA AFDP

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amemwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mwenye hafla ya kupokea magari 4 na pikipiki 16 zilizotolewa kupitia mradi wa kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unaofadhiliwa na mfuko wa kimataifa wa kuendeleza kilimo (IFAD).

Katika hotuba yake wakati wa Hafla hiyo Prof. Shemdoe amesema kuwa Wizara yake inaendelea kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ambapo imelenga kuongeza mchango wa sekta ya Uvuvi kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 1.8 iliyopo hivi sasa mpaka asilimia 10 ifikapo mwaka 2026.

"Kwa hiyo programu hii imekuwa ni chachu ya kuchangia katika mifumo jumuishi ya kuboresha ukuaji wa uchumi kwa wavuvi,wakuzaji viumbe maji na wadau wanaohusika katika mnyororo wa thamani kwenye sekta ya Uvuvi" Ameongezea Prof. Shemdoe.

Aidha Prof. Shemdoe amebainisha kuwa mbali na utoaji wa vyombo hivyo vya usafiri, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya Uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari ya Uvuvi eneo la Kilwa masoko mkoani Lindi ambapo Meli za Uvuvi za kibiashara zitakazonunuliwa kupitia mradi huo kwa ajili ya kuvua katika ukanda wa bahari kuu zinatarajiwa kutia nanga katika bandari hiyo.

"Vyombo tutakavyovipokea leo vitasaidia kuchochea uzalishaji na kuimarisha huduma za ugani kwa kuwafikia wadau wa uvuvi hususan vijana na wanawake" Amesisitiza Prof. Shemdoe.

Vyombo vya usafiri vilivyotolewa leo kupitia Mradi wa kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kwa Wizara zote za kisekta zinazoutekeleza vina thamani ya zaidi ya shilingi Bil.2 na vinatarajiwa kutolewa kwa maafisa ugani ili waweze kuongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

.