SERIKALI YAANZA YAANZA UJENZI WA CHUO CHA MAFUNZO YA MIFUGO SONGWE

Imewekwa: Tuesday 26, March 2024

SERIKALI YAANZA UJENZI WA CHUO CHA MAFUNZO YA MIFUGO SONGWE

◼️ Takribani shilingi Bil.1.2 kutumika mpaka kukamilika kwake

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Wakala yake ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) imeanza ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mifugo katika mkoa wa Songwe kitakachogarimu takribani shilingi Bil.1.2 zilizotolewa na Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni hatua ya kuongeza idadi ya Maafisa Ugani upande wa sekta ya Mifugo nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo kwa Mkandarasi atakayefanya kazi hiyo Machi 25, 2025 Mbozi mkoani Songwe, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Daniel Mushi amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ubora wa majengo unaendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali na kumaliza kazi hiyo kwa wakati waliokubaliana.

“Lakini jambo la msingi zaidi malighafi zote utakazotumia kwenye ujenzi wa chuo hiki zitoke maeneo ya jirani na hili tumekuwa tukisisitiza sana kwenye miradi yetu yote kwa sababu mnafahamu Mhe. Rais anataka kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwenye kuagiza malighafi kutoka nje na tunajua kiasi gani ametengeneza mazingira wezeshi kwa ajili ya wawekezaji hivyo haiingii akilini kusikia mkandarasi ameagiza marumaru kutoka china wakati hapo Mkuranga zipo, wana vioo na alminium pia” Amesisitiza Prof. Mushi.

Kwa upande wake kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbozi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi amewataka wasaidizi wake wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi huyo wakati wote wa ujenzi wa mradi huo huku pia akiahidi kuusimamia kwa karibu na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

“Bahati nzuri mkandarasi upo hapa naomba utimize wajibu wako na ufanye kazi yako kwa sababu mambo ya kuvutana au kukimbizana yameshapitwa na wakati” Ameongeza Mhe. Mgomi.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya “Civil Loth Engineering LTD” Mhandisi Robert Lupinda ambaye ndiye mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ameahidi kukamilisha majengo ya chuo hicho kwa wakati na ubora unaotakiwa huku akiomba ushirikiano wa kutoka kutoka Serikalini wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo.

Kwa Mujibu wa Mhandisi Ujenzi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Mligo, ujenzi huo unajumuisha jengo la Utawala, bweni na chumba cha mafunzo na utakamilika ndani ya miezi 6 kuanzia hivi sasa.

.