PWANI YAHIMIZWA KUTUNZA RASILIMALI ILI KUONGEZA UZALISHAJI SEKTA YA UVUVI

Imewekwa: Saturday 21, September 2024

PWANI YAHIMIZWA KUTUNZA RASILIMALI ILI KUONGEZA UZALISHAJI SEKTA YA UVUVI

Mkoa wa Pwani umehimizwa kutunza rasilimali za mito, maziwa na bahari ili kuongeza uzalishaji wa samaki na mazao mengine yaliyopo katika Bahari ya Hindi.

Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Abubakar Kunenge, amebainisha hayo (20.09.2024) wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuhusisha kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na viongozi wa wilaya kujadili uhifadhi wa bahari kwa vizazi na maendeleo ya sekta hiyo Mkoani Pwani.

Mhe. Kunenge ameeleza kuwa kutunza rasilimali za bahari siyo tu kutaongeza uzalishaji wa samaki bali pia kutaongeza manufaa kwa jamii kupitia shughuli zinazohusiana na uchumi wa buluu.

Amesisitiza kuwa uvuvi ni moja ya sekta muhimu Mkoani Pwani, hasa katika wilaya za Mkuranga, Bagamoyo, Rufiji, Kibiti, na Mafia ambazo ndizo zinazoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya baharini.

Aidha, Mhe. Kunenge ametoa wito kwa Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha halmashauri zinasimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo ya uvuvi.

Pia, amebainisha kuwa endapo usimamizi wa rasilimali za uvuvi utaimarishwa, zitakuwa na manufaa kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa taifa kwa ujumla. Hivyo, sekta ya uvuvi itakuwa endelevu na kubadili mtazamo wa jamii ya wavuvi na wote wanaojihusisha na mazao ya uvuvi.

Amefafanua umuhimu wa kuandaa miongozo ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi na mazingira yake, pamoja na kupanga na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhende, amebainisha kuwa sekta ya uvuvi inachangia asilimia 30 ya protini inayopatikana kwa jamii, ambayo pia ni muhimu kwa kukuza afya ya binadamu.

Ameeleza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa sekta hiyo na kuhakikisha shughuli za uvuvi zinaendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi, kwa lengo la kukuza pato la taifa kupitia Sekta ya Uvuvi.

Dkt. Mhede amesema mkutano huo unalenga kukumbushana majukumu na umuhimu wa kuongeza ufanisi ili ulinzi wa rasilmali za uvuvi unaotakiwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uweze kutekelezwa na kwamba itaendelea kusimamia hilo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Mohamed Sheikh amesema lengo la mikutano ya kukutana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa ni kuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi katika maji yote ya asili zinalindwa ili kuwa na tija katika pato la taifa.

Ameongeza kuwa kumewekwa mikakati mbalimbali ya muda mrefu, mfupi na kati kwa kushirikisha wadau ili kuwa na makubaliano ya pamoja ya namna ya kulinda rasilimali za uvuvi na kuhakikisha rasilimali hizo zinazidi kuzaliana kwa wingi na kuongeza uhitaji katika masoko.

Nao baadhi ya washiriki wamesema mkutano huo umekuja muda muafaka katika kuelimishana na kuwa na mawazo ya pamoja ya kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinazidi kulindwa na kuwa na tija kwa taifa.

.