OPERESHENI ZA KUPAMBANA NA UVUVI HARAMU ZALETA MANUFAA - WAZIRI MKUU

Imewekwa: Wednesday 21, August 2019

Akifunga Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu ‘Nanenane’ yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu, Waziri Mkuu amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuongeza usimamizi na udhibiti wa uvuvi ili kupata pato kubwa la taifa na mtu mmoja mmoja kupitia sekta ya uvuvi.

“Sasa tumeanza kushuhudia kuona ukubwa wa samaki tunaowavua baada ya kuwa pia tumewaacha wakue na tunawavua na wanatuingizia fedha za kutosha haya ni matokeo ya operesheni ambazo tumezifanya”alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema pamoja na operesheni hiyo kufanyika na kuleta manufaa makubwa lakini kulizuka manung’uniko kutokana na usimamizi huo madhubuti uliofanywa na Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu nchini.

“lakini leo hii wavuvi wenyewe wanafarijika kuona kwamba tumepata faida kutokana na operesheni hiyo kwa hiyo Mheshimiwa Waziri (Mpina) endelea kusimamia eneo hili”alisema Majaliwa

Pia ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mpango maalum wa kutoa elimu kwa umma juu ya aina ya nyavu zinazotakiwa zitumike na wavuvi ili kuondoa migongano baina ya wavuvi na Serikali.

Hivyo aliwataka pia wananchi waliohudhuria maonesho hayo kwenda kwenye banda la uvuvi ili kuona aina ya nyavu zinazotakiwa kuvua kwenye maeneo yote ya Mito, Mabwawa, Maziwa na Bahari.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mpina alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa wizara yake itaendelea kusimamia kikamilifu ulinzi wa rasilimali za mifugo na uvuvi na kuhakikishia wafugaji na wavuvi soko la ndani la bidhaa zao halitachezewa tena.

"Wakulima nendeni mkalime, wafugaji nendeni mkafuge, wavuvi nendeni mkavue Serikali iko pamoja nanyi kulinda soko la ndani na Mhe. Waziri Mkuu tumeshakataa kukatishwa tamaa na mtu yoyote na hatutashindwa Serikali ya awamu tano ipo kushughulikia changamoto zenu zote”alisema Mpina.

Mpina alisema mapambano dhidi ya Uvuvi haramu yamewezesha kuongezeka kwa samaki kwenye soko la ndani hivyo kupungua kwa uagizaji wa samaki kutoka nje ya nchi kwa asilimia 67 huku mauzo ya nje yameongezeka kutoka sh. bilioni 379 hadi shilingi bilioni 680.

Pia Operesheni Sangara imefanikiwa kuondoa majini jumla ya nyavu haramu 772,880, Kamba za Kokoro mita 1,970,213, Samaki wachanga na wazazi kilo 568,843, mabondo kilo 6,441 na jumla ya watuhumiwa 9,272 walikamatwa.

Itakumbukwa kuwa Wizara ilikamata jumla ya tani 15.53 za samaki walioingizwa nchini bila nyaraka, leseni na vibali. Samaki hao walipatikana na viambata vya sumu baada ya kufanyiwa uchunguzi ambapo samaki wote waliteketezwa kwa kutokukidhi viwango vya ubora na usalama wa walaji.

Pia Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imefanya utafiti wa kujua rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria kwa kutumia teknolojia ya Hydro-acousti survey kwa kushirikiana na Taasisi za Kenya Marine and Fisheries Research Institute (KMFRI-Kenya) na National Fisheries Resources Research Institute (NaFIRRI-Uganda) ulifanyika mwezi Septemba hadi Oktoba 2018.

Hivyo miongoni mwa matokeo ya utafiti huo ni pamoja na kuwepo kwa ongezeko la Sangara kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi kufikia tani 553,770 mwaka 2018, kupungua kwa Sangara wenye urefu wa chini ya sentimita 50 kutoka asilimia 96.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 62.8 mwaka 2018, kuongezeka kwa Sangara wenye urefu wa kuanzia sentimita 50 hadi 85 kutoka asilimia 3.3 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 32.0 mwaka 2018.

Pia kuongezeka kwa Sangara wenye urefu wa juu ya sentimenta 85 (samaki wazazi) kutoka asilimia 0.4 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2018 na kuongezeka kwa wastani wa urefu wa Sangara kutoka sentimeta 16 mwaka 2017 hadi kufikia sentimeta 25.2 mwaka 2018.

Matokeo hayo yanaonesha kuongezeka kwa Sangara ziwani sambamba na kuongezeka kwa Sangara wazazi na kupungua kwa Sangara wachanga ikilinganishwa na mwaka 2017. Ongezeko hili ni matokeo ya doria na operesheni dhidi ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.

Pia ongezeko hilo la Sangara wakubwa litawanufaisha wavuvi, wenye viwanda na wafanyabiashara ya mabondo kwa vile sangara wenye urefu wa zaidi ya sentimita 85 hutoa minofu na mabondo makubwa ambayo yana thamani ya juu katika soko.

.