NYANDA ZA JUU KUSINI NI ENEO LETU LA KIMKAKATI-PROF. MUSHI

Imewekwa: Tuesday 26, March 2024


NYANDA ZA JUU KUSINI NI ENEO LETU LA KIMKAKATI-PROF. MUSHI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Prof. Daniel Mushi amesema kuwa Wizara yake imeifanya kanda ya Nyanda za Juu kusini kuwa ni eneo lao la kimkakati kwa upande wa Ufugaji hususan ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa.

Prof. Mushi amebainisha hayo leo Machi 25, 2024 wakati akifungua Mafunzo Rejea kwa maafisa ugani wa mikoa iliyopo kwenye kanda hiyo tukio lililofanyika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambapo amesema kuwa licha ya Kanda hiyo kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula kwa ujumla, Wizara yake inaitambua kama kinara wa ufugaji wa ng’ombe bora wa maziwa.

“Wizara yetu ina mashamba 3 ya kimkakati ya kuzalisha mitamba bora na mbegu za malisho ya Mifugo katika kanda hii ya Nyanda za juu kusini ambayo ni shamba la Sao-Hill liilopo Mufindi, Kitulo lililopo Makete na Langwira lililopo Mbarali lakini pia tunazo Taasisi zetu ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo pale Uyole na muda si mrefu tunaenda kuanzisha kituo kipya cha Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Songwe hivyo haya yote ni fursa kwenu maafisa Ugani kufika na kujifunza teknolojia iliyopo kwenye mashamba haya na kutoa ushauri” Ameongezea Prof. Mushi.

Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo Prof. Mushi amesema kuwa ushiriki wa maafisa Ugani kwenye mafunzo hayo utaisaidia Wizara kutafsiri kwa vitendo mipango na mikakati ya Wizara yake katika kuboresha sekta ya Mifugo nchini na kuishusha tafsiri hiyo kwa wafugaji ili waweze kuitekeleza.

“Lakini pia tutakumbushana mgawanyo wa majukumu kati ya Serikali kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo wengi wen undo mpo chini yake ili muweze kujua nafasi yenu katika kutafisiri mipango hiyo ya Wizara” Amesisitiza Prof. Mushi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Songwe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi mbali na kuipongeza Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo amewataka Maafisa Ugani hao kutumia mafunzo hayo kama sehemu ya nyenzo za kwenda kuwafundishia wafugaji ili waweze kufuga kisasa na kwa tija.

“Tunasema Kilimo ni biashara lakini mifugo ni biashara kwa kiwango kikubwa sana na wafugaji ndio matajiri wakubwa lakini wengi wana muonekano wa kimaskini sasa tuna kila sababu ya kuhakikisha tunaleta mapinduzi kwenye sekta ya Mifugo ili iwe na tija katika kuinua uchumi wa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla” Amesema Mhe. Mgomi.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angelo Mwilawa ambao ndio waandaaji wa Mafunzo hayo amesema kuwa jukumu kubwa la Wizara yake ni kuhakikisha maarifa mapya yanawafikia wafugaji wakati wote kupitia kwa maafisa ugani wao huku wakijikita kwenye kuhakikisha wanaongeza elimu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa upande wa sekta ya Mifugo.

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzake, Afisa Ushauri wa Mifugo kutoka Manispaa ya Songea Bw. Edwin Ndunguru ameahidi kwenda kutekeleza kwa vitendo yote waliyoelekezwa huku pia akitoa rai kwa Serikali kuwaandalia mafunzo ya aina hiyo mara kwa mara.

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiendesha Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wote nchini lengo likiwa ni kuhakikisha wafugaji waliopo nchini wanapewa elimu ya mabadiliko ya tekonolojia yanayotokea mara kwa mara ili waendelee kufuga kwa tija.

.