Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
NI LAZIMA TULINDE RASILIMALI ZETU ZA UVUVI KWA WIVU MKUBWA- DKT. KIJAJI

NI LAZIMA TULINDE RASILIMALI ZETU ZA UVUVI KWA WIVU MKUBWA- DKT. KIJAJI
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), ametoa wito kwa Watanzania, hususan wale wanaojihusisha na shughuli za uvuvi kulinda rasilimali hizo za asili ili kuwahakikishia wananchi kukuza uchumi wao kwa misingi endelevu na kuwahakikishia upatikanaji wa malighafi (samaki) wawekezaji wa sekta binfasi waliowekeza kwenye viwanda vya kuchakata samaki na mnyororo wake wa thamani ili kukidhi uwezo wa viwanda hivyo.
Mhe. Dkt. Kijaji ameyasema hayo Disemba 23, 2024 alipotembelea kiwanda cha kuchakata samaki cha Pride of Nile PVT Ltd kilichopo katika Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera ambapo amebainisha kuwa uwekezaji huo ni matunda yanayotokana juhudi za Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kuimarisha mazingira bora na wezeshi sambamba na kuhamasisha sekta binafsi kupanua wigo wa kuongeza thamani ya mazao ghafi ya sekta za uzalishaji, ikiwemo uvuvi.
"Jukumu letu kama Watanzania kwa sasa ni kuzilinda rasilimali hizi za asili kwa wivu mkubwa sana kwa sababu mbali na kutupatia ajira na kipato kwa mtu mmoja mmoja, pia rasilimali hizi zinanufaisha uchumi wa nchi kwa ujumla"
Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji ametoa rai kwa wananchi kuongeza nguvu kwenye ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ili kupumzisha shughuli za uvuvi wa asili na kuwapatia nafasi samaki wa asili (wild fish) wazaliane vya kutosha, sambamba na kumuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza kasi ya uhamaishaji wa ufugaji wa samaki kwa vizimba.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Dkt. Abel Nyamahanga, amesema kuwa asilimia 70 ya eneo la Wilaya hiyo limezungukwa na maji ya Ziwa Victoria na hivyo kufanya sehemu kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Muleba kuwa wavuvi jambo linalowafanya kuwa na kila sababu ya kulinda rasilimali za Ziwa hilo kwa nguvu kubwa.
Akisoma taarifa ya mchango wa kiwanda chao kwenye soko la ajira, Meneja Ubora wa kiwanda hicho, Bw. Mustapha Hamza amesema kuwa kiwanda hicho kimefanikiwa kuajiri Watanzania 125 ambapo pia wanachangia uchumi wa Taifa kwa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali za Serikali. Vile vile, Bw. Hamza alibainisha kuwa upatikanaji mdogo wa malighafi (samaki aina ya sangara) unapelekea kiwanda hicho kutumia chini ya asilimia 50 ya uwezo wake uliosimikwa na hivyo kuiomba Wizara kuja na mkakati shirikishi wa kuhakikisha kunapatikana sangara wa kutosha kwa ajili ya kulisha viwanda ili kukuza mauzo nje na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Awamu ya kwanza ya ziara ya Mhe. Dkt. Kijaji kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa (Mara, Mwanza, na Kagera) ambayo ililenga kufuatilia ufanisi wa sekta, kusikiliza na kupokea changamoto na mapendekezo ya wadau, kuzindua viwanda vya samaki, kuzindua uvunaji wa samaki wafugwao kwa njia ya vizimba kupitia program ya jenga kesho iliyo bora (BBT Life), na kufungua fursa mbalimba zilizopo kwenye sekta ya uvuvi kupitia viwanda vya kuchakata samaki na ukuzaji viumbe maji (hususani samaki aina ya sato) imehitimishwa leo tarehe Desemba 23, 2024 ambapo anatarajia kufanya awamu ya pili ya ziara hiyo mapema mwezi Januari 2025.