MHEDE AAHIDI USHIRIKIANO WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

Imewekwa: Tuesday 23, April 2024

MHEDE AAHIDI USHIRIKIANO WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amehadi ushirikiano kwa watendaji wenzake wa Wizara hiyo.

Dkt. Mhede ameyasema hayo leo Aprili 8, 2024 alipowasili kwa mara ya kwanza katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Jijini Dodoma.

"Mimi siwaahidi nyinyi mambo mengi, ila mimi nawaahidi nyinyi ushirikiano katika kufanya kazi, kama mnakumbuka Mheshimiwa Rais katika kuapishwa kwangu aliniambia nikafanye kazi na kama alivyosema nitafanya kazi maana najua kazi ni ibada na kazi ni takwa la Katiba ya nchi, kwa hiyo nitafanya kazi na nyinyi" amesema Dkt. Mhede

Dkt. Mhede, amemshukuru sana Mungu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mpangaji vikosi kazi.

Akimpokea Naibu Katibu Mkuu Uvuvi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Dkt. Mhede ana bahati naye kufanya nae kazi mahali pengine, kwa maana alivyoteuliwa tu kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara naye Dkt. Mhede alikuwa anaondoka Wizara hiyo lakini baadae wakaja kukutana tena Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati Prof. Shemdoe akiwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI na Dkt. Mhede akiwa Mkurugenzi Mkuu wa DART.

"Wakati tunaagana nilimwambia kuagana ni kukutana tena, na hatukujua kama tutakutana tena, lakini leo hii Mheshimiwa Rais ameona ni vyema kutukutanisha tena kwenye Wizara hii, hii maana yake tunatakiwa kuishi vizuri kwa sababu hatujui kesho tutakuwa wapi na kesho tutakutana tena wapi" amesema Prof. Shemdoe.

.