​MAAFISA UVUVI KAMATENI VIWANDA, MADUKA YANAYOUZA NYAVU HARAMU-MNYETI

Imewekwa: Monday 20, November 2023

MAAFISA UVUVI KAMATENI VIWANDA, MADUKA YANAYOUZA NYAVU HARAMU-MNYETI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amewataka maafisa uvuvi kote nchini kuhakikisha wanapita kwenye viwanda vya ndani na maduka yote yanayouza nyavu za kuvulia samaki zisizoruhusiwa na kuwachukulia hatua za kisheria badala ya kushughulika moja kwa moja na wavuvi wanaozitumia pindi zikiingia sokoni.

Mhe. Mnyeti ameyasema hayo wakati wa hafla ya kugawa boti 9 zenye thamani ya shilingi milioni 535 iliyofanyika Novemba 18, 2023 kwenye mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma ambapo amewataka maafisa uvuvi hao kujenga mazingira ya kuwa karibu na wavuvi ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuwapa elimu juu ya namna bora ya utekelezaji wa uvuvi wa kisasa.

“Tunataka tutoke kwenye dunia ya vuta nikuvute kati ya mvuvi na Afisa Uvuvi kwa sababu mvuvi anapaswa akimuona afisa uvuvi amkimbilie kupata msaada badala ya kumchukulia kama adui” Ameongeza Mhe. Mnyeti.

Mhe. Mnyeti amebainisha kuwa Wizara yake haipendezwi na suala la uchomaji wa nyavu haramu kwa sababu inatambua kuwa wavuvi hao wanategemea shughuli hizo kutimiza mahitaji mbalimbali ya familia zao hivyo amewataka maafisa uvuvi kuhakikisha wanadhibiti maeneo zinapotokea nyavu hizo.

“Maduka tunayajua, wanauza shilingi ngapi tunajua lakini tunasubiri mvuvi akanunue kwa kutoelewa kwake na kumkamata pindi akiziingiza tu kwenye maji, hii si sawa na ni uonevu mkubwa kwa wavuvi hawa” Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa zoezi hilo la ugawaji wa mkopo usio na riba wa boti za uvuvi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Bi. Agness Meena amesema kuwa mkoa wa Kigoma umepewa boti 9 kati ya 160 zinazotolewa kwa wanufaika wa mkopo huo nchini nzima ambapo zote kwa pamoja zina thamani ya Bil. 11.5.

“Mpango huu unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na boti 92 zinatolewa kwa ukanda wa Pwani na nyingine 68 zinatolewa kwa ukanda wa maji baridi” Amesema Bi. Meena.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa boti ya kisasa ya uvuvi na vifaa vyake, mmoja wa wanufaika wa mkopo huo kutoka wilaya ya Uvinza Bi. Ester Bugegene ameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono kupitia mkopo huo ambapo ameiomba kuendelea kuwawezesha wakati wote watakapohitaji kuongezewa nguvu kwenye utekelezaji wa shughuli zao za uvuvi.

Utekelezaji wa mpango wa ugawaji wa boti za kisasa za Uvuvi ni miongoni mwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan za kuhakikisha sekta ya uvuvi inakuwa na mchango mkubwa kwenye kukuza pato la Taifa na mvuvi mmoja mmoja.

.