LUSHOTO MMEMTENDEA HAKI DKT. SAMIA- DKT. KIJAJI.

Imewekwa: Friday 10, January 2025

LUSHOTO MMEMTENDEA HAKI DKT. SAMIA- DKT. KIJAJI.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Lushoto kwa usimamizi mzuri wa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Wilayani humo.

Dkt. Kijaji ametoa pongezi hizo wakati akihitimisha ziara yake ya siku 2 Wilayani humo ambapo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kulinda miradi hiyo ili fedha nyingi zilizotolewa na Serikali katika ujenzi wake isipotee.

"Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alinituma nije Wilayani Lushoto kukagua na kuona namna pesa aliyolenga ije kutekeleza miradi ilivyotumika na leo kwa furaha kabisa tena huku nikijivunia kazi nzuri niliyoiona ntamueleza pesa yake imesimamiwa vema na imetumika vizuri kabisa hapa Wilayani Lushoto" Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji amempongeza Mbunge wa jimbo la Mlalo Mhe. Dkt. Rashid Shangazi kwa juhudi zake za kuwaombea wananchi wake fedha za miradi ya Maendeleo ambapo amewataka wananchi wa jimbo hilo kujivunia kuwa na kiongozi wa aina hiyo.

Akijibu changamoto ya bei ndogo ya maziwa wanayolipwa wafugaji wa Wilaya hiyo waliopo kwenye vyama vya msingi, Mhe. Dkt. Kijaji ameielekeza Bodi ya Maziwa nchini kufika Mlalo ndani ya wiki mbili kuanzia leo kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.

Mara baada ya kumaliza ziara yake Wilayani Lushoto Mhe. Kijaji anatarajia kuendelea na ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi ya Maendeleo katika Wilaya ya Korogwe.

.