KONGAMANO LA KITAIFA LA NGURUWE KUFANYIKA TANZANIA

Imewekwa: Wednesday 16, April 2025

Na. Chiku Makwai (MUV). Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na chama cha wafugaji wa Nguruwe Tanzania (TAPIFA) imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la ufugaji wa nguruwe litakalo fanyika Septemba 11-13, 2025 jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Aprili 16, 2025 na Naibu Waziri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti Wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari Uliofanyika katika Ukumbi uliopo jengo la NBC jijini Dodoma.

Mhe. Mnyeti amesema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 2000 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wakiwemo Viongozi wa Serikali na Wizara za kisekta, Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, Vijana na Wanawake, Wanataaluma, Wadau wa Maendeleo, Wafugaji na Wafanyabiashara katika mnyororo wa thamani wa Nguruwe.

Aidha, ameongeza kuwa kongamano hilo litaambatana na Mafunzo kutoka kwa wataalam na Wadau wa Maendeleo katika tasnia ya Nguruwe, pia washiriki kufanya majadiliano ya kibiashara na kuzitambua fursa zilizopo Kitaifa, Kikanda na Kimataifa pamoja na kutembelea uwandani kwa wadau kujionea namna ufugaji wa kisasa wa Nguruwe unavyofanyika.

Mhe. Mnyeti amebainisha kuwa ufugaji wa Nguruwe unaendana na malengo ya nchi katika kuhimiza maendeleo ya sekta ya mifugo ili kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na Nguruwe.

.