​KIWANDA KIKUBWA CHA KUCHAKATA SAMAKI KUJENGWA NCHINI

Imewekwa: Monday 27, November 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kufuatia sera nzuri za kuvutia uwekezaji za Serikali ya Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan zimeifanya Kampuni ya Albacora kutoka nchini Hispania kuja hapa nchini kujenga kiwanda kikubwa cha kisasa cha kuchaka samaki ambacho kitakuwa cha kwanza katika Ukanda Pwani ya Bahari.

Waziri Ulega amesema hayo wakati akifanya ukaguzi wa meli hiyo na kupokea Tani Hamsini (50) ya samaki wasiolengwa walioletwa na kampuni hiyo ya Albacora, leo jijini Dar es Salaam Novemba 23, 2023.

"Mhe. Rais anavutia zaidi sekta Binafsi kufanya kazi za uwekezaji hapa nchini ili iwe injini ya uwekezaji, biashara na uzalishaji na ndio maana kampuni ya Albacora wako tayari kuwekeza hapa nchini na tayari wameshanunua eneo Mkoani Tanga kwa ajili ya kujenga kiwanda hicho kitakachotoa ajira ya moja kwa moja kwa vijana wa kike na kiume wasiopungua mia moja," alisema Waziri Ulega

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, Kampuni ya Albacora imepewa leseni ya Tanzania kuvua samaki aina ya Jodari katika bahari kuu na makubaliano ni kwamba wakipata samaki mwingine tofauti na Jodari wanapaswa kuwarudisha hapa nchini.

Alifafanua kwa kusema kuwa jitihada za Mhe. Rais, Dkt. Samia za kujenga bandari ya uvuvi ya Kilwa Masoko kutawezesha meli nyingi kubwa kama hizo za Albacora kutoka nje ya nchi kutia nanga hapa nchini na hivyo kutaharakisha kuchechemua uchumi wa nchi yetu kwa kiasi kikubwa kupitia uchumi wa buluu.

.