WAZIRI KIJAJI AIPA HEKO MIRADI YA MAENDELEO WILAYANI LUSHOTO

Imewekwa: Tuesday 07, January 2025

WAZIRI KIJAJI AIPA HEKO MIRADI YA MAENDELEO WILAYANI LUSHOTO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga kuangalia thamani halisi ya pesa zilizoletwa katika miradi hiyo.

Akizungumza wakati akizindua mradi wa ujenzi wa barabara ya Njia Panda kutoka Hospitali ya Wilaya ya Lushoto hadi Kijiji cha Kwembago kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa Moja, amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutawezesha wananchi kuondokana changamoto ya barabara waliyokuwa wakikabiliana nayo.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema ujenzi wa barabara hiyo uliyogharimu zaidi ya Shilingi Milioni 490, kutawezesha wananchi kufika katika hospitali hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa urahisi hususan nyakati za mvua.

Pamoja na kuzindua barabara hiyo, Mhe. Dkt. Kijaji amekagua mradi wa uzalishaji mbegu za vifaranga vya samaki aina ya sato, kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mabweni mawili Shule ya Sekondari Shambalai na ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike Shule ya Sekondari Kwalei pamoja na kuzindua huduma ya usafiri wa wagonjwa na kukabidhi gari ya wagonjwa.

.