ELIMU KUTOLEWA KWA WANUFAIKA WA BOTI KANDA YA ZIWA VICTORIA

Imewekwa: Thursday 04, July 2024

ELIMU KUTOLEWA KWA WANUFAIKA WA BOTI KANDA YA ZIWA VICTORIA

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza mchakato wa kutoa elimu kwa wanufaika wa Boti kanda ya ziwa Viktoria mkoani Mwanza na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakumba wanufaika hao, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwasikiliza na kushughulikia changamoto zao na kutoa elimu za utumiaji Boti 55 hizo zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, januari 30 mwaka huu zenye thamani zaidi ya Bilioni 2. Hii ni kufuatia kujua changamoto zinazowakumba wanufaika hao licha ya kupata mafanikio mengi kupitia mradi huo.

Akizungumza, leo Juni 21, 2024 Mkoani Mwanza wakati alipowatembelea wanufaika wa boti kanda ya ziwa Viktoria ili kujua hali ya shughuli za uvuvi kwa wanufaika hao, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwin Mhede amesema Wizara imeamua kuanza kutoa elimu kwa wanufaika wa boti kanda ya ziwa Viktoria ili kuwapatia ujuzi zaidi katika utumizi wa boti hizo na vifaa vyake vya uvuvi.

"nimeshatoa maelekezo kwa niaba ya serikali, kwamba Chuo cha Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi-FETA, pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo-TALIRI kwamba tushirikiane na Taasisi za Serikali zilizopo Mwanza hususani Shirika la Uwakala ya Meli Tanzania-TASAC, pamoja na Halmashauri ya Mji Mwanza kwa maana ya TAMISEMI na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB katika kutoa elimu kwa wanufaika wa boti kuhusu Mradi huu na kuwasikiliza ikiwemo kuwahudumia pia", amesema Dkt. Mhede

Aidha, Dkt. Mhede alisema yeye na wataalamu wenzake wa Wizara ya Mifugo na uvuvi pamoja na kutoa elimu kwa wanufaika wa boti, pia watakaa pamoja ili kujadili ni jinsi gani wataweza kutatua changamoto zinazowakabili wanufaika hao na baadae kuja kuwapa mrejesho na kutekeleza kwa kushughulikia changamoto zao mbalimbali zinazowakabili wanufaika hao.

Kwa upande wake, Meneja wa kanda Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB, Bw. Alphonce Mokoki amesema kuanzia mwezi julai, TADB itaanza kuwatembelea wanufaika wa boti kanda ya ziwa ili kufanya maongezi nao na kutoa elimu ya mikopo ya Boti hizo na kutatua changamoto zao.

Vilevile Bwana Mokoki amesema TADB iko tayari kushauriana na wanufaika kwenye swala la marejesho ya mkopo na swala la mnufaika wa mkopo wa boti kuchukua mkopo katika benki zingine.

Akitoa ufafanuzi juu kifaa cha kuonyesha kusaidia kupata samaki kijulikanacho kama Fish Finder, Mkaguzi wa vyombo na Mtaalamu Mitego ya Uvuvi - TASAC, Naodha Marwa amesema TASAC kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaandaa elimu juu ya utumizi wa kifaa hicho kwa wanufaika wa boti.

Naye, Mnufaika wa mradi wa boti za uvuvi, zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa vikundi mbalimbali vya uvuvi kanda ya ziwa, Mwenyekiti BMU Makuyuni, Bw. Robert Charles amesema, boti hizo za kisasa zimewasaidia kufungua fursa za upatikanaji wa ajira na kuwakwamua kiuchumi, kupitia ongezeko la uvunaji wa samaki.

Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwakumbuka na kusema, serikali ya awamu ya sita ndiyo pekee imewajali kupitia sekta ya wavuvi. Na kuomba kuwaongezea vifaa vya uvuvi ikiwemo nyavu za dagaa na taa pamoja na mashine na kuendeshea boti hizo.

.