DKT. MHEDE APONGEZA HIYARI YA UPUMZISHAJI ZIWA IKIMBA

Imewekwa: Sunday 22, December 2024

DKT. MHEDE APONGEZA HIYARI YA UPUMZISHAJI ZIWA IKIMBA

◼️ Wizara yajipanga kuwasaidia kupumzisha kitaalam awamu ijayo

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amewapongeza wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye Ziwa Ikimba kwa uamuzi wao wa kufunga shughuli za Uvuvi wa ziwa hilo kwa hiyari.

Dkt. Mhede ametoa pongezi hizo leo Disemba 22, 2024 baada ya kufika kata ya Kaibanja lilipo ziwa hilo ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo inatokana na matokeo chanya yaliyopatikana baada ya upumzishwaji wa Ziwa Tanganyika.

Aidha Dkt. Mhede ameziagiza Taasisi zilizopo chini ya Sekta yake kuhakikisha kila moja inashiriki kikamilifu kutoa ushauri wa kitaalamu na nyenzo zitakazowasaidia kupumzisha kwa tija pindi watakapofanya hivyo kwa awamu nyingine.

Akizungumzia hatua itakayochukuliwa na Taasisi yake katika kuhakikisha upumzishwaji wa Ziwa hilo unakuwa na tija Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) Kituo cha Mwanza Dkt. Benedicto Kashindye amesema kuwa Taasisi yake itafanya utafiti wa aina ya samaki wanaopaswa kupandwa ziwani hapo huku pia wakishirikiana na Wavuvi kuhakikisha wanashauri njia sahihi za Uvuvi ili kuondokana na Uvuvi haramu.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala ya Mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) kampasi ya Nyegezi Bw. Peter Masumbuko amesema kuwa Taasisi yake itawapeleka wataalam kwa ajili ya kutoa elimu na kupandikiza vifaranga vya samaki pindi utafiti wa aina ya samaki wanaoweza kukua katika ziwa hilo utakapokamilika.

Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Bi. Gracious Malugu amesema kuwa mara baada ya TAFIRI kujiridhisha uwezekano wa ufugaji samaki kwa njia ya Vizimba katika ziwa hilo, Benki yao kupitia kiasi cha Bilioni 1 kilichotengwa kwa mkoa wa Kagera itaviwezesha vikundi vya wanawake na vijana mkopo huo wenye masharti nafuu wa Vizimba vya kufugia samaki ili waweze kufanya shughuli hiyo katika ziwa hilo.

Wavuvi wa Ziwa Ikimba lenye ukubwa wa kilomita za mraba 38.09 wapo tayari kupumzisha ziwa hilo ambapo wanatarajia kujikita kwenye shughuli za kilimo wakati wote wa upumzishwaji huo.

.