DKT. KIJAJI AWATAKA WATUMISHI WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KUWA WAZALENDO

Imewekwa: Friday 28, March 2025

◼️Ataka watumishi kuwatumikia vyema wananchi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa na utumishi wa kizalendo uliotukuka kwa Watanzania ili kuweza kusongambele katika Sekta hizo mbili.

Akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo leo Machi 26, 2025 katika Kikao chake na watumishi hao, kilicho jumuisha Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Wizara, kilichofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Wizara katika Mji wa Kiserikali Mtumba, Dkt. Kijaji amesema anafurahishwa sana na utendaji mzuri wa watumishi wa Wizara hiyo huku akiwapongeza kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.

"wizara inaonekana jinsi inavyofanya kazi na inaendelea kufanya kazi vyema kwani tangu tuanze kuzunguka na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, tulikopita kwenye Miradi yetu yote walitupongeza na kusema tumefanya vizuri" amesema Dkt. Kijaji.

Aidha, Dkt. Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Vilevile, Dkt. Kijaji amesema matarajio na matumaini ni makubwa katika Sekta za Mifugo na Uvuvi kwa sababu Mheshimiwa Rais tangu aingie madarakani ameamua kuzipa kipaumbele Sekta za uzalishaji ikiwemo Sekta hizi mbili, ambazo ndio Sekta zinazogusa maisha ya kawaida ya Watanzania na hakuna nyumba utakayokwenda ukakosa Mifugo au mvuvi, kila siku ya mungu Sekta hizi mbili lazima ziguswe, na ni Sekta zinazogusa watu wa chini kabisa.

Aidja, Dkt. Kijaji amewaelekeza Watendaji wa Wizara kuhakikisha wanasimamia maeneo yote ya Mifugo na Malisho na kuainisha maeneo hayo pamoja na kuwaita wafugaji kuwaelewesha umuhimu wa kumiliki ardhi na malisho.

Halikadhalika, Dkt. Kijaji watendaji wa wizara kuanza zoezi ra kuwarasimisha wavuvi wote nchi na kuwatambua wapo wangapi na wanafanya nini, ikiwa ni pamoja na kujua kuwa kuna vyombo vingapi vya uvuvi nchini.

"Wakuzaji Viumbe Maji tuwe na tathimini ya maji yote na kuamua kufanya kazi ipasavyo ili ndani ya miaka 5 ijayo pato kubwa la nchi hii litokane na uchumi Buluu, na hilo linawezekana." amesema Dkt. Kijaji

.