Nifanyeje?
- Zipi sifa za kuorodheshwa kama msaidizi wa mtaalam wa mifugo? (Enlisted Paraprofessional Assistant)
- Zipi sifa za kujiandikisha kama mtaalam msaidizi wa mifugo? (Enrolled Paraprofessional).
- Daktari wa mifugo asiye mtanzania (Foreigner) anasajiliwa vipi na Baraza.
- Daktari wa mifugo asiye Mtanzania anaweza kusajiliwa na kufanyakazi hapa nchini? (Temporary and permanent registration)?
DKT. KIJAJI ADHAMIRIA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA MIFUGO

DKT. KIJAJI ADHAMIRIA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA MIFUGO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amedhamiria kuboresha miundombinu ya ufugaji ili wafugaji wafuge kisasa wakiwa katika maeneo yao rasmi na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama.
Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha hayo leo (Januari 04, 2025) wakati wa kikao chake na baadhi ya wafugaji katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro ambapo amesema katika kuhakikisha hilo ni lazima wakuu wa mikoa wahamasishe mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Ameongeza kuwa kufuatia mpango huo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inadhamiria bajeti zake za fedha za kila mwaka zitoe vipaumbele kwenye malisho ya mifugo na maji ili kuwaondolea adha wafugaji kutotembea muda mrefu kufuata mahitaji hayo muhimu kwa ajili ya mifugo yao.
"Tumeanzia Morogoro kuleta mbegu za malisho ya mifugo ili wafugaji wawe na maeneo yao rasmi kwa ajili ya kilimo cha malisho ya mifugo. " Amesema Mhe. Dkt. Kijaji
Aidha, amefafanua kuwa katika Mwaka wa Fedha 2025/26 serikali itakuja na mpango kwa ajili ya kuchimba visima na mabwawa ili kuwahudumia wafugaji na mifugo yao kote nchini.
Pia, amesema vituo atamizi na mbegu bora za mifugo ndiyo chachu kwa Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kuuza mazao ya mifugo nje ya nchi na kuondokana na vikwazo vya kimataifa ambavyo imekuwa ikikabiliana navyo juu ya ubora wa mazao hayo yanapotakiwa katika nchi hizo.
Baadhi ya wafugaji waliohudhuria kikao hicho wamempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyoleta matokeo chanya kwa wafugaji kwa kuwahimiza kufuga kisasa na kuwasogezea huduma mbalimbali karibu na maeneo yao.