CHANJO YA MIFUGO SASA NI LAZIMA SIO HIYARI-MNYETI

Imewekwa: Wednesday 13, December 2023

CHANJO YA MIFUGO SASA NI LAZIMA SIO HIYARI-MNYETI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema kuwa kuanzia mwezi Julai mwakani (2024) chanjo za kuikinga mifugo na magonjwa mbalimbali itakuwa ni lazima na sio hiyari kama ilivyo sasa.

Mhe. Mnyeti amebainisha hayo Disemba 13, 2023 wakati akifungua mkutano wa 41 wa Wataalam wa wanyama nchini (TVA) unaofanyika jijini Arusha ambapo ameongeza kuwa hatua hiyo imetokana na kubainika kwa ukosefu wa soko la nyama inayozalishwa hapa nchini huku sababu kubwa ikielezwa ni wingi wa magonjwa yanayoathiri mifugo.

“Leo hata ukizunguka kwenye hoteli kubwa hapa Tanzania watakuambia nyama yao wanaagiza kutoka Afrika Kusini ukiuliza sababu watakuambia ni usalama mdogo wa nyama yetu kutokana na magonjwa ya mifugo na ukiuliza unaambiwa chanjo hapa kwetu ni hiyari , sasa hili hatuwezi kukubali liendelee” Amesisitiza Mhe. Mnyeti.

Mhe. Mnyeti amesema kuwa mbali na manufaa ya kiuchumi, hatua hiyo inalenga kulinda afya za walaji wa ndani pia ambao mara nyingi wamekuwa wakiathiriwa na maradhi yanayotokana na mifugo ukiwemo ugonjwa wa kutupa mimba.

“Yaan kama ambavyo binadamu akizaliwa tu anapewa chanjo za maradhi kama polio, surua, pepopunda na mengineyo, tunataka na wanyama wachanjwe kuanzia wanazaliwa mpaka wanachinjwa” Amesema Mhe. Mnyeti.

Katika hatua nyingine Mhe. Mnyeti amewataka wataalam hao wa wanyama kutekeleza wajibu wao na kuachana na majukumu ambayo yapo nje ya taaluma zao ili wawe msaada kwa wafugaji wa maeneo waliyopo.

“Kuna wengine jukumu lao kubwa ni kukamata mifugo inayozurula hovyo jambo ambalo kitaaluma sio kazi yao na wengine wamekuwa maafisa watendaji wa kata na ndio maana hata idadi ya wataalam waliohudhuria hapa ni ndogo kwa sababu wengine wameona ni bora kuendelea kukaimishwa kuongoza kata kuliko kuja kwenye mkutano wao wa kitaaluma” Amesema Mhe. Mnyeti.

Akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Chama cha wataalam wa wanyama (TVA) Prof. Esron Karimuribo amesema kuwa kongamano hilo hufanyika kwa lengo la kuwakutanisha wataalam mbalimbali wa wanyama ambao hujadili mambo mbalimbali yanayolenga kuboresha ustawi wa wanyama nchini na hivyo kuchangia uboreshaji wa mazao yatokanayo na wanyama hao kama vile nyama, maziwa, ngozi na mengineyo.

.