BBT-LIFE SASA NI ZAMU YA TASNIA YA KUKU

Imewekwa: Friday 08, December 2023

BBT-LIFE SASA NI ZAMU YA TASNIA YA KUKU

Mikoa kinara kupewa zawadi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe ameagiza kuanzishwa kwa programu ya “Jenga kesho iliyo njema” (BBT) kwa upande wa Tasnia ya kuku ili kuongeza wigo wa ongezeko la ajira kwa wanawake na vijana kote nchini.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati ya kufuatilia makubaliano kati ya Wizara na wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa Kuku iliyofanyika Disemba 12,2023 jijini Dodoma ambapo amewataka Maafisa mifugo wa mikoa yote nchini kuwaainisha wadau waliopo kwenye mikoa yao na kuanza utekelezaji wa programu hiyo.

“Sekta hii ndogo ya kuku kwa sasainajumuisha watu wengi sana na bahati nzuri fedha za kuwawezesha vijana na wanawake hawa watakaoingia kwenye programu ya BBT zipo kwenye Halmashauri zenu kupitia asilimia 10 ya wanawake, vijana na wenye ulemavu hivyo nendeni mkawajengee uwezo ili waanze kufuga mara moja” Amesema Prof. Shemdoe.

Aidha Prof. Shemdoe ameongeza kuwa Serikali itatoa motisha kwa Mikoa na maofisa mifugo waliopo kwenye mikoa itakayoongoza kwa utekelezaji wa programu hiyo ili kuongeza chachu ya utekelezaji wa program hiyo na hatimaye iweze kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.

Akielezea namna walivyopokea maelekezo hayo Afisa Mifugo wa mkoa wa Katavi Bw. Zidhery Mhando amesema kuwa mkoa wake ulishaanza ngazi ya awali ya utekelezaji wa program hiyo kwa kuwaainisha wadau wa tasnia ya kuku waliopo mkoani humo huku pia akisisitiza kuwa watahakikisha sekta hiyo inakuwa na mchango mkubwa zaidi kwa mfugaji mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Awali akiwasilisha taarifa fupi ya maendeleo ya Tasnia ya kuku nchini mmoja wa wadau wakubwa wa sekta binafsi kutoka kampuni ya “AKM Glliters” Bi. Elizabeth Swai amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikumba tasnia hiyo ni kasi ya ukuaji wa teknolojia ambayo sehemu kubwa ya wafugaji wameshindwa kuendana nayo kutokana na kuwa na mitaji midogo.

Uanzishwaji wa program ya “Jenga kesho iliyo njema” kwa upande wa Tasnia ya kuku inakuja mara baada ya mafanikio yaliyoonekana kwenye utekelezaji wa programu hiyo kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi ambapo vijana na wanawake wamefanikiwa kuwa wajasiriamali kwenye sekta hizo.

.