WANAOLIMA MAENEO YA MALISHO, WAONYWA WAONDOKE
Wafugaji na wakulima wanaolima kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo wametakiwa kuondoka mara moja kwenye maeneo hayo ili yatumike kama ilivyokusudiwa.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amebainisha hayo leo (17.12.2025), wakati wa ziara yake ya kikazi alipozungumza na wananchi wengi wao wakiwa ni jamii ya wafugaji kwenye kongani za malisho katika Kijiji cha Engang’uengare kilichopo Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, baada ya kubainika kuwepo kwa shughuli za kilimo katika maeneo hayo.
Baada ya kusikiliza kero zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa vijiji na wananchi Mhe. Kamani amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada za kudhibiti migogoro ya wakulima na watumiaji wengine wa ardhi huku ikibainika baadhi ya wafugaji kushiriki katika shughuli za kilimo maeneo ya malisho.
Ameongeza kuwa ni wajibu kwa serikali na wafugaji wenyewe kuheshimu na kulinda maeneo ya malisho na wasiwe mstari wa mbele katika kukiuka sheria za nchi.
Katika hatua nyingine Mhe. Naibu Waziri ameshiriki zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa kwa Bw. Sayei Mussa ambaye ni mmoja wa wafugaji wakubwa katika Kijiji cha Orkitikiti na kubainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga Shilingi Bilioni 216 kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kwa ajili ya chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa.
Aidha, ameongeza kuwa chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa ni muhimu katika kuiongezea thamani mifugo hususan kwenye zao la nyama kwa soko la nje ya nchi, hivyo serikali itahakikisha wafugaji wengi wanafikiwa ili kushiriki zoezi hilo muhimu kwa taifa.
Amefafanua kuwa ni muhimu wafugaji kumuunga mkono Mhe. Rais ili kufikia maono ya kutokomeza magonjwa dhidi ya mifugo, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri Wilaya ya Kiteto kwenye chanjo za kimkakati katika wilaya hiyo kwa Mwaka 2024/2025 ng’ombe 184,673 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu, mbuzi 62,746 dhidi ya ugonjwa wa sotoka na kuku 188,197 dhidi ya ugonjwa wa kideri.
Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Naibu Waziri Kamani, amearifiwa na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Remedius Mwema kwamba ofisi yake imekuwa ikitoa elimu kwa wafugaji kutenga maeneo ya malisho pamoja na kuwachukulia hatua wale wanaovamia maeneo yasiyotakiwa kisheria ili kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Pia, kuhusu chanjo ya utambuzi wa mifugo kitaifa, Bw. Mwema amesema wilaya yake inazidi kuweka mikakati mbalimbali ya kuwafikia wafugaji kutokana na tafiti kuonesha bado baadhi ya wafugaji hawajafikiwa kwa muda unaotakiwa.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Manyara, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani amekabidhi pikipiki tatu (3) kwa maafisa ugani wa zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa ili kuongeza wigo wa kuwafikia wafugaji wengi zaidi.
Katika maeneo mbalimbali ya ziara yake, Mhe. Naibu Waziri Kamani amepokea maoni ya wananchi hususan wafugaji kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji ya kutosha, majosho na mbegu za malisho huku akiahidi serikali kuendelea kutatua changamoto hizo kwa kushirikiana na wananchi.