Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AWATAKA WAUZA NYAMA NJE YA NCHI KUUNGANA

Imewekwa: 11 February, 2026
DKT. BASHIRU AWATAKA WAUZA NYAMA NJE YA NCHI KUUNGANA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewataka wauzaji wa nyama nje ya nchi kuunda umoja imara utakaowawezesha kufanya biashara kwa tija na kuhimili ushindani wa kimataifa.

Akizungumza Februari 11, 2026 katika kikao na wadau hao kilichofanyika Hoteli ya Gerwill, Dodoma, Dkt. Bashiru alisema umoja huo utarahisisha mawasiliano na Serikali na kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Pia amesisitiza umuhimu wa kuendesha biashara kwa uendelevu ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kutosha viwandani.

“Katika uchumi wa kisasa wenye ushindani mkali, hasa katika masoko mnayolenga, mnashindana na nchi ambazo zimewekeza kwa muda mrefu. Hakuna njia ya mkato. Nawashauri kikao hiki kiwe chimbuko la wazo la kuunda umoja imara wa wauza nyama nje ya nchi, ambao utarahisisha mawasiliano kati yenu na Serikali,” amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alisema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kitaifa wa chanjo za mifugo, kuboresha kosafu na kuhamasisha ufugaji wa kisasa ili kuongeza thamani ya tasnia ya nyama.

Awali akiwasilisha taarifa ya hali ya Tasnia ya Nyama, Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Bw. John Chassama, kuanzia Julai 1, 2025 hadi Januari 30, 2026 Tanzania iliuza tani 9,325.8 za nyama nje ya nchi zenye thamani ya Dola za Marekani 39,459,370.71.

Wauzaji wa nyama wameeleza changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo masuala ya sera, sheria, usafirishaji na mitaji, na kuiomba Serikali na taasisi za fedha kushirikiana nao ili kukuza biashara hiyo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo