BI. MEENA AWATAKA WATUMISHI KUWA NA USHIRIKIANO MADHUBUTI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness Meena amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuwa na ushirikiano madhubuti na kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha utendaji kazi na kufikia malengo ya Sekta kwa ufanisi zaidi.
Bi. Meena ametoa wito huo leo Februari 11, 2026 kwenye ofisi ya Makao Makuu ya Wizara iliyopo Mji wa Kiserikali Mtumba Dodoma, wakati wa hafla ya kuwakaribisha Manaibu Makatibu Wakuu wapya wa wizara hiyo.
“Nitumie nafasi hii kuwasihi watumishi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi ili kufanikisha malengo tuliojiwekea,” amesema Bi. Meena.
Katika hafla hiyo, Bi. Meena amemshukuru aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo kwa mchango wake katika kuendeleza sekta na kuwapongeza viongozi wapya kwa kuaminiwa kushika nyadhifa hizo muhimu katika wizara.
Aidha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Edwini Mhede amesema katika kipindi chake alichokuwa hapa Wizarani amejifunza mambo mengi kuhusu sekta za mifugo na uvuvi, akitoa shukrani dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Wizara kwa ushirikiano waliompa.
Pia amesisitiza kuwa walifanya kazi kindugu, n kwa kushirikiana, kusaidiana, na kuahidi kuwa ana imani kubwa na viongozi wapya katika kuendeleza majukumu ya Wizara.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Mifugo), Dkt. Fabian Madele amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyoonesha kwake, na kuahidi kusimamia sekta ya mifugo kwa weledi, kuzingatia misingi ya kisayansi na kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wote.
Naye Naibu Katibu Mkuu (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh amesema dhamana aliyopewa ni deni linalopaswa kulipwa kwa utendaji kazi bora katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050 na kukuza uchumi wa buluu.
Aidha, Prof. Sheikh amesisitiza kuwa utumishi wa umma ni kama mbio za kupokezana vijiti hivyo ni zamu yao sasa kufanya kazi kwa bidii, umoja na upendo huku wakiondoa majungu na chuki mahali pa kazi ili kujenga mazingira bora ya utendaji.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko Nchini, Ndg. Stephen Michael amesema kuwa watumishi wa wizara wataendelea kutoa ushirikiano wa dhati na kufanya kazi kwa kitimu ili kuhakikisha wizara inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.