​WANANCHI MBARALI WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI

Imewekwa: Wednesday 18, January 2023

  • Wasema sasa wapo huru kuendelea na shughuli zao za ufugaji na kilimo kwa amani.

WANANCHI wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 15 na hivyo kuwawezesha kuendelea kufanya shughuli zao za ufugaji na kilimo kwa uhuru na amani.

Wamesema kumalizika kwa mgogoro huo ambao ulihusisha wakazi wa wilaya hiyo wanaoendesha shughuli za ufugaji na kilimo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumanne, Januari 17, 2023) baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwatangazia wananchi hao kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye Tangazo la Serikali namba 28 na kuliacha nje ya mpaka wa hifadhi eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 74,000 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi hao kufanya shughuli za ufugaji na kilimo. Mkutano huo umefanyika kijijini Kapunga.

“Tunamshukuru mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia kwa uamuzi mkubwa alioufanya wa kuboresha GN 28, sasa tutafuga kwa uhuru na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama, pia tunamshukuru kwa uamuzi wa serikali wa kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija watakayopatiwa ambayo inakwenda kuwasaidia kuongeza mnyororo wa thamani” Amesema Mwenyekiti wa Wafugaji katika ranchi ya Matebele-Madunguru, Lokordu Siloma.

Kadhalika amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi na sasa wanakwenda kufuga kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa. “Awali watu wenye uwezo walikuwa wanavamia maeneo ya ranchi na kuendesha shughuli za kilimo lakini kwa kauli hii wafugaji tutaachiwa ranchi zetu tulishe mifugo yetu. Tunaishukuru sana Serikali.”

Naye Elibauti Mwinuka mkulima katika kata ya Itamboleo wilayani Mbarali amesema kuwa sasa watalima kwa uhuru na kuongeza uzalishaji kwa sababu awali tulikuwa tunalima kwa wasiwasi.

Anle Kifute ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kapunga amesema amefurahishwa na kauli ya Serikali ambayo inakwenda kuwaondolea migogoro katika maeneo yao na hivyo wataweza kuendesha shughuli zao bila ya usumbufu wa aina yoyote.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Majaliwa baada ya kutangaza maamuzi hayo ya Serikali, amewataka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Zuberi Homera na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune wahakikishe wanasimamia vizuri sheria pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki pamoja na viongozi wa Ranchi za Taifa waende kwenye Ranchi ya Usangu na kuwapanga upya wafugaji ili manufaa ya ufugaji yaonekane ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.

Amesema Serikali imefanya maboresho hayo kwa lengo la kuwawezesha wafugaji na wakulima wilayani humo kuendesha shughuli kitaalamu na kuwaongezea tija. “Marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka na kutumiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo.”

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amemuhakikishia Waziri Mkuu kuwa Wizara itakwenda kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa juu ya matumizi ya Ranchi ya Usangu ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wale wote wanaoitumia ranchi hiyo kinyume na makubaliano yaliyowekwa.

Aidha, amesema kuwa Wizara itashirikiana na wafugaji kuhakikisha miundombinu ya ufugaji unajengwa na kuboreshwa katika eneo hilo.

.