KAMANI AWAONESHA FURSA WAWEKEZAJI SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, akiahidi ushirikiano wa Serikali katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki na wezeshi.
Mhe. Kamani ametoa kauli hiyo leo, Septemba 17, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara maalum ya kikazi ya kutembelea wawekezaji wanaofanya shughuli katika Sekta za Mifugo na Uvuvi.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri ametembelea Kampuni ya Alphakrust Limited pamoja na Kampuni ya Farmbase, ambapo amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanyika katika sekta hizo.
Amesema Serikali imedhamiria kushirikiana kwa karibu na Sekta binafsi katika kukuza Sekta za Mifugo na Uvuvi, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Kamani amesema Serikali inaendelea kuweka mifumo inayorahisisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi, ili kuongeza uzalishaji, kuchochea uwekezaji na kuimarisha mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa.
Aidha, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 unalenga kuongeza nafasi ya Sekta binafsi katika kujenga uchumi wa Taifa, ambapo Serikali imejipanga kushirikiana na wawekezaji kufikia malengo hayo.
“Serikali ipo bega kwa bega na Sekta binafsi kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki na wezeshi,” amesema Mhe. Kamani.
Amebainisha kuwa Tanzania ina fursa nyingi katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, huku akiwataka wawekezaji kuzitumia fursa hizo katika kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa zinazotokana na sekta hizo.
Mhe. Kamani pia ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwemo upatikanaji wa ardhi, mitaji pamoja na mifumo ya kodi inayolenga kuwezesha uwekezaji nchini.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza Sekta za Mifugo na Uvuvi na kuongeza manufaa yake kwa Taifa.