Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. MADELE AHIMIZA MABADILIKO MRADI WA MAGEUZI YA TASNIA YA MAZIWA

Imewekwa: 17 September, 2026
DKT. MADELE AHIMIZA MABADILIKO MRADI WA MAGEUZI YA TASNIA YA MAZIWA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Fabian Madele amewataka watekelezaji wa mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi kuhakikisha hatua ya pili ya utekelezaji wa mradi huo inawagusa wafugaji moja kwa moja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao kazi cha wadau wanaotekeleza mradi huo Dkt. Madele amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo kwa mwaka uliopita ulijikita zaidi kwenye maandalizi ya miongozo hivyo ana imani hatua iliyobaki kwa sasa ni kwenda uwandani kwa wafugaji.

“Lengo letu hapa ni kuweka alama ya mabadiliko ya Tasnia ya Maziwa kwa kiwango tulichowdka kwenye malengo na kutengeneza mifumo ambayo inahimili mabadiliko ya tabianchi kwa sababu huyu mfugaji tunayemuongelea hayupo hapa Dodoma mjini bali yupo huko Rungwe, Kilolo na kwingineko” Amesema Dkt. Madele.

Aidha Dkt. Madele amewataka wataalam hao kupunguza vikao na kuelekeza nguvu uwandani ili kutambua wahusika wa mradi, wanachofanya na wanachopaswa kusaidiwa.

Kwa upande wake mratibu wa Mradi huo Dkt. Lazaro Kapella amesema kuwa mradi huo una maeneo 26 ya utekelezaji hivyo kila mdau anayehusika na mradi huo anapaswa kuongeza kasi kwenye utekelezaji wake.

“Asilimia zaidi ya 70 ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/2027 ni manunuzi hivyo nitoe wito kwa watekelezaji wa mradi wahakikishe wanaharakisha taratibu zote za manunuzi kwa sababu walishapata mafunzo” Amesema Dkt. Kapella.

Kikao hicho kitahitimishwa Septemba 18,2026 ambapo hatua inayofuata baada ya hapo ni utekelezaji wa mradi huo kwa wahusika uwandani.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo