WAFUGAJI WATAKIWA KUMILIKI MAENEO NA KUPANDA MALISHO

Imewekwa: Monday 16, January 2023

Wafugaji wilayani Tarime wametakiwa kumiliki maeneo na kupanda majani kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.

Hayo yamesemwa leo (08.01.2023) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashamba Ndaki alipokuwa anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Karekatonga wilaya ya Tarime mkoa wa Mara baada ya kusikiliza kero zao.

Waziri Ndaki amesema kuwa wafugaji wanatakiwa kubadilika na kuanza kufuga kisasa na kibiashara kwa kuhakikisha mifugo wanayofuga inapata malisho ya kutosha kulingana na maeneo wanayoyamiliki pamoja na huduma za mifugo.

Malisho ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wafugaji wengi na hivyo kusababisha mifugo kufa hasa kipindi cha ukame. Hivyo wafugaji wameshauriwa kumiliki mifugo inayoendana na eneo la malisho wanayomiliki.

Vilevile Waziri Ndaki amekemea vikali suala la upigwaji risasi mifugo linalodaiwa kufanywa na askari wa wanyamapori. Wananchi katika vijiji vinavyoizunguka Mbuga ya Serengeti wamelalamikia tatizo hilo na hivyo kumuomba Mhe. Waziri kuwasaidia wafugaji hao.

Aidha, Waziri Ndaki amekemea vikali suala la mifugo kupigwa risasi kwa kuwa lipo kinyume na sheria zinazolinda mifugo hapa nchini. Hii ni kutokana na wananchi hao kulalamika kuhusu mifugo yao kupigwa risasi na askari wa wanyamapori.

Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara amesema kuwa serikali katika jimbo hilo imefanya mambo mengi ya maendeleo lakini wananchi wameomba suala la alama za mipaka kati ya vijiji na eneo la hifadhi ya Serengeti liwekwe wazi ili kuondoa migogoro iliyopo sasa kati ya wafugaji na askari wa wanyamapori.

.