DKT. NCHEMBA AVUTIWA NA VIWANGO BANDARI YA UVUVI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amevutiwa na viwango vya ujenzi wa bandari ya Uvuvi inayokamilishwa ujenzi wake Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
Mhe. Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa bandari hiyo Desemba 19,2025 ambapo amesema kuwa bandari hiyo ya uvuvi ni mwanzo wa safari ya utekelezaji wa miradi mikubwa iliyoandikwa kwenye DIRA 2050.
"Bandari hii ni mojawapo ya miradi mingi inayofafanua kauli za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizozitoa baada ya kuapishwa kwamba atasimamia utekelezaji wa miradi inayotoa majibu ya kero za Watanzania," Amesema Mhe. Dkt. Nchemba
Aidha Dkt. Nchemba ameongeza kuwa mbali na ujenzi wa bandari hiyo Serikali ipo mbioni kununua meli tano za uvuvi zitakazoongeza kiwango cha mavuno ya samaki ili kuharakisha ukuaji wa sekta ya uvuvi.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa watahakikisha bandari hiyo inazalisha ajira, mapato na inaendelea kuwa kielelezo cha mafanikio ya Serikali.
"Kwa vile bandari hii ni ya kisasa, tumeanza mchakato wa kuithibitisha katika viwango vya kikanda na kimataifa hivyo ninawakaribisha wadau kutoka sekta binafsi kwani wana nafasi kubwa ya kuwekeza kwenye eneo la mafuta (ya boti), viwanda vya uchakataji samaki na uendeshaji wa bandari hiyo.” Amesema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa bandari hiyo, Msimamizi wa mradi huo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhandisi George Kwandu alimweleza Waziri Mkuu kwamba mradi huo umefikia asilimia 90 mpaka sasa na utagharimu kiasi cha sh. bilioni 280 hadi kukamilika kwake.
"Mradi huu una eneo la ekari 48. Gati yenye urefu wa mita 315 ambayo ina uwezo wa kupaki meli 10 na zikashusha mzigo kwa wakati mmoja na Jengo hilo likikamilika tutaweza kuhifadhi tani 1.8 za samaki kwa wakati mmoja na kuzalisha tani 100 za barafu kwa siku ambayo ni mahitaji makubwa ya wavuvi kwa sasa.” Ameongeza Mhandisi Kwandu.
Mradi huo unaotarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya Uvuvi nchini unatarajiwa kukamilika na kuzinduliwa mwishoni mwa mwezi Machi 2025.