Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mifugo na Uvuvi

DKT. BASHIRU AALIKA WAWEKEZAJI WA NDANI UFUGAJI SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA

Imewekwa: 23 December, 2025
DKT. BASHIRU AALIKA WAWEKEZAJI WA NDANI UFUGAJI SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewataka wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa nyingi zilizopo kwenye tasnia ya ufugaji wa samaki.
 
Balozi Dkt. Bashiru amesema hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wavuvi mkoani Mara Desemba 22,2025 ambapo amewataka wawekezaji hao kuelekeza macho yao kwenye fursa za Viwanda vya vyakula vya samaki, uzalishaji wa vifaranga vya samaki na mikopo kwa vikundi vinavyofanya shughuli hizo za ufugaji wa samaki.

“Ufugaji wa samaki ni utajiri na ndio maana pamoja  na changamoto zilizopo bado hakuna ambaye yupo tayari kuacha kufanya shughuli hiyo hivyo niwaalike wawekezaji hasa wa ndani kwa sababu kwenye eneo la kuzalisha vifaranga tunataka tuwe na wawekezaji ambao watahakikisha vinapatikana wakati wote na wapo ambao kwa uwezo wao wa kimtaji wameshafikia katika hatua mbalimbali” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru amesisitiza kuwa tasnia hiyo ni kielelezo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliiasisi kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi wanawake na vijana kupitia sekta ya Uvuvi hivyo ambapo amewataka watu wote kuchangamkia fursa hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani ambaye alikabidhiwa kusimamia makundi ya vijana na wanawake wanaojihusisha na sekta za Mifugo na Uvuvi amesema kuwa ripoti zinaonesha kuwa kundi la vijana na wanawake wameanza kunufaika na programu hiyo ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ambapo ameahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ili kuendelea kuyanufaisha kiuchumi makundi hayo.

Naye mmoja wa wanufaika wa programu hiyo amesema kuwa wafugaji wote walionufaika na mikopo ya vizimba hivyo katika awamu ya kwanza walifanikiwa kuvuna samaki wengi na kurejesha fedha za mikopo hiyo licha ya changamoto kadhaa walizokumbana nazo kutokana na kukosa uzoefu.

Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Naibu wake Mhe. Ng’wasi Kamani itaendelea Desemba 23,2025 katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo