DKT. BASHIRU AWAPIGIA CHAPUO WAFUGAJI KUPATA MIKOPO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amesema kuwa Serikali inakusudia kuweka utaratibu utakawawezesha wafugaji kupata mikopo kupitia Taasisi za fedha nchini kama ilivyo upande wa Wakulima.
Balozi Dkt. Bashiru amebainisha hayo Januari 09,2026 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wavuvi nchini.
“Wakulima wanakopeshwa lakini mara chache sana wafugaji kukopeshwa na kama huwezi kukopesheka ni vigumu sana kupiga hatua kubwa lakini tatizo tulilonalo mabenki yetu gharama za mikopo zipo juu watu wanaogopa kufilisiwa” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.
Aidha Balozi Dkt. Bashiru amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha mikopo itakayotolewa kwa wafugaji inakuwa ya gharama nafuu kwa upande wa riba huku pia ikiwa na uwezo wa kulipwa hatua ambayo ameeleza kuwa itawasaidia wafugaji hao kufuga kisasa.
Mbali na kuzungumza na wafugaji na wavuvi wa Wilaya ya Ushetu, Balozi Dkt. Bashiru pia alitembelea na kukagua kiwanda kinachotarajiwa kusindika maziwa cha Jambo ,Machinjio ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Eneo la kupumzishia Mifugo la Chibe.