​UPUMZISHWAJI ZIWA TANGANYIKA UMEONGEZA MALIGHAFI VIWANDANI- DKT. KIJAJI

Imewekwa: Friday 24, January 2025

UPUMZISHWAJI ZIWA TANGANYIKA UMEONGEZA MALIGHAFI VIWANDANI- DKT. KIJAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa zoezi la upumzishwaji wa hiyari wa shughuli za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika limechagiza ongezeko kubwa la malighafi za Viwanda vilivyopo kwenye mikoa inayozungukwa na ziwa hilo.

Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha hayo Januari 23, 2025 mara baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kuchakata samaki cha "Alpha Tanganyika" kilichopo mkoani Rukwa ambapo amemwelekeza mwekezaji wa Kiwanda hicho kuanza shughuli za uchakataji mara moja.

"Tunataka hivi viwanda viwe vitengeneze ajira kwa vijana wetu na najua hapo awali sababu yako kubwa ilikuwa ni kutopata malighafi za kutosha kulingana na uwezo wa kiwanda chako lakini kwa sasa kupitia zoezi la Upumzishwaji wa ziwa samaki wameongezeka kwa zaidi ya tani 15,000 ukilinganisha na tani 4,700 za mwaka 2023 mpaka wafanyabiashara wamekosa masoko ya kupeleka samaki hao hivyo wewe anza na sisi tutabeba changamoto za kisera ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji wako yanakuwa bora" Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake Mmiliki wa Kiwanda hicho Bw. Alpha Nondo mbali na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa alioupata amesema kuwa kiwanda chake kitakuwa cha kwanza nchini kuchakata samaki kutoka ziwa Tanganyika na Victoria kwa wakati mmoja.

"Tayari tuna ithibati kutoka soko laUmoja wa Ulaya na Marekani hivyo tunaamini tukianza kazi uchumi wa watu wa Rukwa utaimarika" Amesema Bw. Nondo.

.